
Mkoa wa Morogoro leo Juni 8, 2026 umepokea Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 ambazo zinatarajiwa kukimbizwa katika Halmashauri tisa za Mkoa huo kwa lengo la kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Jumla ya miradi 63 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 50.9 itatembelewa na Mwenge huo Uhuru katika kipindi cha mbio hizo.

Mwenge wa Uhuru umepokelewa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, katika tukio liliofanyika mkoani humo baada ya kuwasili ukitokea Mkoa wa Dodoma.
Mapokezi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa huo wa Morogoro.
Akiupokea Mwenge huo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema Mwenge wa Uhuru ni chombo muhimu cha kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini.
Aidha, amewataka wananchi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Mwenge na kulinda mafanikio ya miradi inayotekelezwa kwa manufaa ya jamii.
Ukiwa Mkoani humo mwenge wa uhuru utakimbizwa umbali wa Km 1898 na utakabidhiwa Mkoa wa Tanga tar.17 Juni, 2026









