Na Adery Masta.
Katika hatua muhimu ya kuendelea kulinda afya za wananchi pamoja na kuimarisha ubora wa huduma za chakula mitaani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo Mei 25, 2026 limetoa mafunzo maalum kwa wafanyabiashara wa chips jijini Dar es Salaam, yakilenga kuimarisha usalama, usafi na ubora wa chakula hicho kinachopendwa na maelfu ya wakazi wa jiji hilo.
Mafunzo hayo yamekuja wakati ambapo biashara ya chips imeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku kwa wananchi wengi, hususan nguvu kazi ya Taifa inayotegemea chakula hicho kwa urahisi na upatikanaji wake wa haraka katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema ni muhimu kwa wafanyabiashara wa chips kuzingatia viwango vya usafi na usalama wa chakula ili kulinda afya za walaji pamoja na kujenga imani kwa wateja wao.
Dkt. Katunzi alisisitiza matumizi sahihi ya mafuta ya kukaangia, akieleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiongeza mafuta mapya kwenye mafuta yaliyokwisha haribika kutokana na matumizi ya muda mrefu, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa kiafya kwa watumiaji wa chakula hicho.
Alieleza kuwa matumizi ya mafuta kwa muda mrefu bila kuyabadilisha huongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuathiri ubora wa chakula kinachotolewa kwa wananchi.
Mbali na hilo, Mkurugenzi huyo wa TBS aliwataka wafanyabiashara hao kuzingatia ufungashaji salama wa chakula hicho maarufu, kuhakikisha chips zinapakiwa katika mazingira safi na salama yanayozingatia afya ya mlaji wa mwisho.
Katika moja ya maeneo yaliyopokelewa kwa uzito mkubwa na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Katunzi aliwahimiza wafanyabiashara hao kuanza kutumia Nishati Safi ya kupikia, akieleza kuwa hatua hiyo si tu inalinda afya zao na mazingira, bali pia inaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanatumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.
Alibainisha kuwa matumizi ya nishati safi yatasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi, kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyabiashara pamoja na kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya nishati zisizo salama.
Hatua ya TBS kutoa mafunzo hayo imeonekana kuwa ni mwendelezo wa juhudi za taasisi hiyo katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa na huduma zinazokidhi viwango vya ubora na usalama, huku ikiendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara nchini.
Wafanyabiashara walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza TBS kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu, wakisema itawasaidia kuboresha huduma zao, kulinda afya za wateja wao pamoja na kukuza biashara zao kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.























