Na Mwandishi Wetu.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uzingatiaji wa viwango katika uzalishaji wa bidhaa na huduma ni msingi muhimu wa kulinda afya za wananchi, kukuza biashara, kuimarisha viwanda vya ndani na kujenga uchumi endelevu wa taifa.
Chalamila ameyasema hayo katika hafla ya Viwango Marathon iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo, akieleza kuwa tukio hilo limebeba ujumbe mpana unaogusa afya za wananchi, mshikamano wa kijamii, uwajibikaji wa taasisi na maendeleo ya taifa.
Amesema mbio hizo si maadhimisho ya kawaida bali ni maadhimisho yenye maono yanayoshirikisha jamii kwa njia bunifu ya kufikisha elimu kuhusu umuhimu wa viwango kwa wananchi katika maisha yao ya kila siku.
“Kuandaliwa kwa Viwango Marathon ni ubunifu mkubwa unaolenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa viwango huku pia tukikuza afya na mshikamano wa kitaifa. Bila viwango hatuwezi kujenga uchumi imara na endelevu,” amesema Chalamila.
Aidha, amesema sekta ya viwanda na biashara haiwezi kustawi bila uwepo wa viwango bora vinavyolinda afya na usalama wa wananchi pamoja na kuwezesha ushindani katika masoko ya kimataifa.
Pamoja na hayo amewahimiza wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi kutumia bidhaa zilizoidhinishwa na TBS huku akiwataka washiriki wa marathon hiyo kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya bidhaa zenye viwango katika familia, biashara na jamii kwa ujumla.
Pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa taasisi kama TBS ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kusaidia viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika katika soko la kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi TBS, Prof. Othman Chande amesema kuwa katika kipindi cha miaka 50, TBS imeendelea kutekelezamajukumu yake ya msingi ya kuandaa na kusimamia viwangokwa lengo la kulinda afya na usalama wa walaji, kuwezeshamazingira ya usawa katika biashara, pamoja na kukuzaushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na njeya nchi.
Kupitia jitihada hizi, TBS imekuwa chombo muhimu katikamaendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini, sambambana kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi waviwanda.
Nae Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema tukio hilo pia linaendana na Mpango Mkakati wa TBS, hususan katika eneo la ustawi wa watumishi na jamii, ikiwa ni pamoja na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo yanayosababishwa na mtindo wa maisha usio na mazoezi.
“Tunaamini kuwa afya bora ni mtaji wa taifa, na mtumishi mwenye afya ni msingi wa tija, ubunifu na utoaji wa huduma bora”. Amesema
Amesema mbio hizo zimebeba Kaulimbiu isemayo “Quality for Every Step, Safety for Every Stride” . kauli mbiu hii ina ujumbe mzito kwani hii inamaanisha Kila hatua ya maendeleo inahitaji ubora, na kila safari ya maisha inahitaji usalama. Hivyo ndivyo TBS inavyojikita katika kulinda na kuimarisha viwango vya maisha ya watanzania.





























