
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameendelea kutoa mchanganuo wa mafanikio ya serikali bungeni leo, Mei 11, 2026, akibainisha kuwa nchi imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa dawa na kuimarisha nguvu kazi.
Katika wasilisho la Bajeti ya Wizara ya Afya, Mchengerwa ameeleza kuwa upatikanaji wa dawa muhimu sasa umefikia asilimia 88, huku serikali ikiajiri wataalamu wa afya zaidi ya 53,000 ndani ya miaka mitano.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya umeimarika kote nchini kupitia MSD ikiwamo uwekezaji wa Trilioni 1.4 katika kununua bidhaa za afya (Trilioni 1.1) na kupambana na UKIMWI, Malaria, na Kifua Kikuu (Bilioni 141.9).
Aidha, amesema serikali imevutia uwekezaji wa viwanda 11 vya dawa na vifaa tiba, ikiwemo juhudi za kuufufua kiwanda cha TPI Arusha ili kuanza kuzalisha dawa za VVU nchini.
Aidha, serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuongeza idadi na ubora wa watumishi ambapo jumla ya wataalamu 53,633 wameajiriwa kuanzia mwaka 2021 hadi Machi 2026, kupitia Samia Health Super Specialization Scholarship, wataalamu 2,982 wamepelekwa masomoni kupata ubingwa bobezi, ongezeko kubwa ikilinganishwa na wataalamu 961 wa kipindi kilichopita.








