Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kupata huduma za msaada wa kisheria zitakazoanza kutolewa kuanzia tarehe 6 hadi 20 Mei 2026, kwa muda wa siku kumi na tano katika halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 5, 2026 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhita amesema huduma hizo zinatolewa bure kabisa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili, yenye lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wenye uhitaji wa msaada wa kisheria.
Amesisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zikiwemo migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa na mirathi, pamoja na haki za msingi, bila kulazimika kugharamia huduma hizo.
“Tunawaomba wananchi wote wa Shinyanga kutumia fursa hii muhimu kujitokeza kwa wingi ili kupata msaada wa kisheria bila malipo. Hii ni nafasi ya kipekee inayolenga kuwasaidia kupata haki zao kwa urahisi,” amesema Mhita.
Aidha, amebainisha kuwa wataalamu wa sheria watakuwepo katika halmashauri zote za mkoa huo kwa kipindi chote cha kampeni, kuhakikisha kila mwananchi anayehitaji msaada anafikiwa kwa wakati.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, hasa wale wa maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha kila mmoja anapata fursa sawa ya kupata haki kwa mujibu wa sheria.








