Home Kitaifa EACCA YAAPISHA MAKAMISHNA WAPYA, WAAHIDI KUSIMAMIA USHINDANI WA HAKI KATIKA SOKO

EACCA YAAPISHA MAKAMISHNA WAPYA, WAAHIDI KUSIMAMIA USHINDANI WA HAKI KATIKA SOKO

Katika hatua kubwa inayolenga kuleta mapinduzi kwenye soko huria na kumlinda mlaji, Mamlaka ya Ushindani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCA) zimekutana mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, na kuwaapisha rasmi wajumbe wapya wanne kutoka nchi za Tanzania, Somalia, Uganda na DRC.

Wajumbe hao watasimamia mazingira mazuri ya ushindani wa biashara na kulinda walaji katika jumuiya hiyo. Waliapishwa kuanza safari ya miaka minne ya uongozi, nao ni Bi. Khadija Ngasongwa (Tanzania), Bw. Zackey Kalega (Uganda), Bw. Ahmed Warsame (Somalia) na Bw. Dolly Kenga (DRC).

Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, amesema watahakikisha mazingira bora ya biashara kwa wafanyabiashara wa jumuiya hiyo pamoja na kulinda walaji dhidi ya mbinu potofu sokoni.

Aliongeza kuwa wamepewa dhamana ya kusimamia sera na sheria zinazolinda ushindani wa biashara na kuwatetea watumiaji kote katika kanda ya Afrika Mashariki.

Kuapishwa kwa makamishna hao kunakuja katika kipindi ambacho biashara kati ya nchi wanachama inaendelea kushamiri, hali inayohitaji usimamizi imara. Mamlaka hiyo inatarajiwa kuwa mlinzi mkuu wa walaji na kusimamia ushindani wa haki katika soko la kikanda.

Aidha, uwepo wa safu mpya ya uongozi unatoa ishara kwa wawekezaji wa kimataifa kuwa ukanda wa Afrika Mashariki umeimarika kisheria na uko tayari kwa biashara yenye uwazi na ushindani wa kimataifa.

Mamlaka hiyo inafanya kazi chini ya Sheria ya Ushindani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2006.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!