Home Kitaifa VITONGOJI VYOTE MKOA WA KILIMANJARO SASA KUWA NA UMEME

VITONGOJI VYOTE MKOA WA KILIMANJARO SASA KUWA NA UMEME

Wananchi katika vitongoji 186 ambavyo vinatarajiwa kupelekewa umeme Mkoani Kilimanjaro wamehamasishwa kuanza kufanya maandalizi ya kuupokea mradi huo kwa kuanza kutandaza nyaya ndani ya nyumba zao (wiring).

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Kilimnajrao, Mhe. Nurdin Babu wakati wa kikao cha kumtambulisha mkandarasi, Derm Group (T) Limited alieshinda zabuni ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 186 vya Mkoa huo katika kipindi cha miaka mitatu.

Mradi huo wa kupeleka umeme katika vitongoji unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 33.5.

Kuanza kwa mradi huo wa kupeleka umeme katika vitongoji 186, kutaufanya Mkoa wa Kilimanjaro kuwa na umeme katika vitongoji vyake vyote 2,258.

“Tunamshkuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake njema ya kutaka kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wote wanapata nishati ya umeme mpaka kwenye ngazi ya kitongoji.

Mkoa wa Kiliamanjaro tunaenda kuandika historia kuwa miongoni mwa mikoa 3 inayokwenda kufikisha umeme katika vitongoji vyake vyote. Hii ni heshima kubwa sana. Nitumie fursa hii kuwahamasisha wananchi kuanza kufanya maandalizi ya kupokea umeme pindi mkandarasi atakapoanza kazi rasmi kwa kufanya wiring kwenye nyumba zao,” amesema Mhe. Babu.

Mkuu huyo wa Mkoa pia ametoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa umeme kwa kuanzisha biashara mbalimbali ili lengo la serikali la kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme liweze kutimia.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha, CPA. Daniel Mungure ametoa wito kwa wananchi kumpa ushirikiano mkandarasi pindi atakapoanza kutekeleza mradi lakini pia kulinda miundombinu ya umeme ambayo imejengwa kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake Meneja wa kampuni ya Derm Group, Mhandisi Musa Abdallah ameahidi kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa kimkataba na kwamba atashirikiana karibu na viongozi na wananchi wa maeneo ya mradi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!