Wananchi Mkoani Geita watakiwa kuchangamkia fursa ya umeme kwenye Vitongoji vyao ambapo Wakala ya Nishati Vijijini (REA) inatarajia kusambaza umeme kwenye vitongoji 528 vitakavyo fikia jumla ya kaya 17,014 Mkoani humo.
Hayo yamesemwa leo tarehe 30/01/2026 Mkoani Geita na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela wakati wa kumtambulisha mkandarasi alieshinda zabuni hiyo, kampuni ya Central Electricals International Ltd itakayotekeleza Mradi huu wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 528 vya mkoa wa Geita kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mhe. Shigela amesema niwakati sahihi kwa Wananchi wa Mkoa huo kuchangamkia fursa hiyo na umeme usiwe tu kwa ajili ya kuchaji simu, kupiga simu na kuchati bali ikawe ni chachu ya kuongeza uzalishaji kwenye maeneo yao na itawapunguzia gharama walizokuwa wakiingi hapo awali.
“Fursa hii inayopatikana ya kuwa na Nishati, sio tu kwaajili ya kuchaji simu ili uweze kuchati, kupiga simu lakini vilevile umuhimu wake ni kuongeza uzalishaji kwenye maeneo yetu” amesema Mhe. Shigela
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa, wakulima waliokuwa na uhitaji wa mashine zinazotumia umeme sasa watanunua mashine na kuongeza thamani ya uzalishaji wa mazao na kwa wale wachimbaji wa dhahabu waliokuwa wakisumbuliwa na maji kwenye Maeneo ya uchimbaji wa madini (Mashimo) sasa watavuta umeme ili waweze kutoa maji hayo kwenye mashimo kwa urahisi zaidi.
“Wananchi wetu waliokuwa wanazalisha na kufanya uchimbaji wa dhahabu, wanasumbuliwa na maji kwenye maduara yao. Sasa umeme unasogea watavuta ili kutoa maji na hivyo kuwasaidia kuchimba kwa urahisi” amesema Mhe. Shigela .
Kwa upande wake, Mhandisi Seif Abdul Mhandisi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amesema kuwa Mradi huo unahusisha upelekaji wa Umeme katika Vitongoji 528 vya Mkoa wa Geita ambapo hapo awali havikuwa na Umeme.
Ameongeza kuwa, mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Central Electricals International Ltd ambaye atajenga 663KM za Msongo wa kati na 821KM za Msongo Mdogo na kuunga wateja 17,014
Pia, Mhandisi Seif amesisitiza kwa Wananchi wa Mkoa huo kuchangamkia uwepo wa kifaa kinachoitwa OMETA ambapo kitawasaidia wananchi waishio Vijijini wasio na uwezo wa kusambaza nyaya ndani ya nyumba (Wiring) kuunganishiwa umeme kupitia kifaa hicho.
Aidha, amebainisha bei elekezi ya Serikali kwa Umeme wa Njia moja ni Tsh. 27000 na Umeme wa njia tatu ni Tsh. 139000.

















