Na Magreth Mbinga
Chama Cha ACT WAZALENDO kimesema Serikali imetekeleza baadhi ya mapendekezo ambayo waliyapendekeza ikiwemo kutoa ruzuku ya mbolea, kuondoa kodi kwenye mafuta ya kula na kupunguza tozo za miamala ya kielektroniki yaani tozo za simu na miamala ya kibenki.
Hayo yamezungumzwa na Waziri Mkuu kivuli wa Chama hiko Ndg Dorothy Semu katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao makuu ya Chama Magomeni Jijini Dar es Salaam.

“Mwenendo wa mfumuko wa bei za bidhaa bado ni kizungumkuti na hali ya maisha ya watu itazidi kuwa mbaya ifikapo mwaka 2023 hivyo ACT WAZALENDO tunaitaka Serikali kuweka mikakati kuhami maisha ya watu na kujiandaa kukabiliana na hali hiyo na kuwaandaa wananchi kuongeza uzalishaji au kukidhi mahitaji ya ndani”amesema Semu.
Pia Dorothy amesema kwa muda wa miezi kumi wamekuwa mstari wa mbele katika kufanya mageuzi ya sheria ya Jeshi la Polisi ili kufanya Jeshi kuwa na weledi ,kujali wananchi na kutokuwa Jeshi la mabavu dhidi ya raia.
“Tulifanya uchambuzi wa bajeti na kutoa mapendekezo yetu wakati wa uchambuzi wa bajeti Serikali izingatie athari za kibajeti sinazotokana na mchakato wa mageuzi wa Jeshi la Polisi “amesema Semu.
Aidha Semu amesema walipigania mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ilikuifanya tume ya Taifa ya uchaguzi kufanya mageuzi ya kidemokrasia na uendeshaji wa siasa zao .

“Tumeshuhudia vilio vya wananchi kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji kwa maeneo ambayo hayakuwa na mivutano hiyo hususa ni Mikoa ya Kusini ,tulitahadhalisha hali ya wakulima na wafugaji inahatarisha amani ya Nchi yetu “amesema Semu.
Sanjari na hayo Semu amesema migogoro hiyo ni bomu ambalo linenda kulipuka siku za usoni hivyo Serikali ilipe uzito unaostahiki ikiwemo kwa Wakuu wa Wilaya wenye uwezo mkubwa wa kutatua migogoro kwa njia ya amani badala ya kutumia nguvu za dola.
“Ni rai yetu kwamba viongozi wawekeze nguvu kwenye kuleta mshikamano kwa kusimamia mipango shirikishi ya ardhi,kushughulikia watendaji na viongozi wote wanaopokea rushwa ,kutoza fidia za uongo ili kupora haki za wakulima na Jeshi la Polisi lisimamiwe vya kutosha kushughulikia matukio ya uhalifu na uhujumu wa Mali za wakulima “amesema Semu.