
Kariakoo, 18 Juni, 2026
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kariakoo imewapongeza walipakodi wa eneo la Mchikichini kwa mchango wao mkubwa ambao umekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Mamlaka, katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.
Kupitia ulipaji wa kodi kwa hiari na ushirikiano wao wa karibu na TRA, walipakodi hao wameendelea kuchangia ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa huduma za kijamii na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Leo na Kaimu Meneja wa TRA Kariakoo Bw. Edson Issanya alipotembelea Kijiwe cha Mchikichini ikiwa ni sehemu ya shughuli za maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na kampeni ya kuwashukuru walipakodi kwa mchango wao mkubwa uliowezesha Mamlaka kufikia mafanikio mbalimbali tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996.
Akizungumza Wakati wa ziara hiyo Bw. Issanya alisema, “Tunalo Dawati la Uwezeshaji Biashara maalum kwa kukwamua changamoto za kikodi na kurahisisha upatikanaji wa suluhisho kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na biashara.
Niwaondoe hofu wafanyabiashara; fika ofisi za TRA, eleza changamoto yako na tutashirikiana kuitatua.
Pia, nawaomba muwe mabalozi kwa wengine kwa kuhamasisha kuwa ofisi za TRA ziko wazi na tayari kuboresha huduma kwa walipakodi wote.,”
Ziara hiyo pia ilitoa fursa kwa walipakodi kusikilizwa, kutoa maoni yao na kujadiliana na maafisa wa TRA kuhusu namna ya kuendelea kuboresha huduma za kodi.
Hatua hiyo inaendana na dhamira ya TRA ya kuweka mlipakodi katikati ya huduma zake na kuimarisha uhusiano wa karibu na wadau wake.
Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yanaendelea nchini kote kupitia shughuli mbalimbali za kuwafikia walipakodi, kutambua mchango wao na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake katika Siku ya Mlipakodi tarehe 1 Julai 2026, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.









