
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emanuel Tutuba amesema kuwa Noti Mpya za Tanzania zenye Saini ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia Februari mosi mwaka huu.
Gavana Tutuba amesema hayo leo Januari, 22,2025 jiji Dar es Salaam wakati akimkabidhi Dk. Nchemba, Noti kifani za shilingi elfu kumi, elfu Tano, Elfu Mbili na Shilingi Elfu moja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
“Waziri ninayofuraha kukujulisha kuwa zoezi letu la uchapaji upya wa Noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la Serikali,” amesema Tutuba.
Amefafanua kuwa Noti hizo zitatumika sambamba na Noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa Noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais Dk. Philip Isdor Mpango imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Dk. Mwigulu Nchemba na Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Profesa Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Emmanuel Tutuba,” ameongeza Tutuba.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za Noti hizo mpya, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa Noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,” amesema Dk. Nchemba.
Pia ameridhia Noti hizo ziingizwe kwenye mzunguko na kuanza kutumika kama ilivyopangwa tarehe moja Februari mwaka huu.