Dar es Salaam.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, amezindua Mwongozo wa Hatua kwa Hatua wa Ufanyaji Biashara chini ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), ambapo amesema soko hilo ni fursa muhimu kwa Tanzania kupanua masoko ya bidhaa zake, kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa za ndani.
Amesema Tanzania imeendelea kutekeleza makubaliano ya AfCFTA, ikiwemo kushiriki katika Mpango wa Majaribio wa Biashara (Guided Trade Initiative) mwaka 2022 na kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa makubaliano hayo na kuongeza kuwa zaidi ya kampuni 40 za Kitanzania zinasafirisha bidhaa katika zaidi ya nchi 16 za Afrika, zikiwemo Ghana, Morocco, Algeria, Nigeria na Misri.
Amesisittiza kuwa AfCFTA ni fursa halisi inayopaswa kutumiwa na wafanyabiashara kuongeza mauzo na kupanua biashara zao na kuongeza kuwa mwongozo huo unaleta matokeo kwa taasisi za Serikali kuutumia kutoa elimu na ushauri kwa wafanyabiashara; Wataalamu wa Wizara za Tanzania Bara na Zanzibar kushirikiana na sekta binafsi kuusambaza na kuuweka kwenye tovuti; Vyama vya wafanyabiashara kuhakikisha unawafikia wanachama wao moja kwa moja; Na wafanyabiashara, hususan wanawake na vijana, kuutumia kutafuta wanunuzi wapya na kupanua biashara zao. Ameongeza kuwa mwongozo huo unapaswa kuwa wa vitendo na kusasishwa kila mara kunapotokea mabadiliko ya taratibu na taarifa za biashara.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi, amesema mwongozo huo umeandaliwa kujibu changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu masoko ya Afrika, taratibu za biashara, masharti ya ubora na nyaraka zinazohitajika kwa wafanyabiashara. Ameeleza kuwa mwongozo huo umeandaliwa kwa Kiswahili na Kiingereza ili kurahisisha upatikanaji na uelewa wa taarifa hizo kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara.
Manongi amesema kufunguliwa kwa soko la AfCFTA pekee hakutoshi kuhakikisha Tanzania inanufaika, bali kunahitajika bidhaa zenye ubora na ushindani, wazalishaji wenye uwezo na wafanyabiashara wenye maarifa ya kutumia fursa zilizopo. Ameeleza kuwa mafanikio ya mwongozo huo hayatapimwa kwa idadi ya nakala zitakazosambazwa, bali kwa idadi ya wafanyabiashara watakaoutumia kufikia masoko mapya na ongezeko la bidhaa za Tanzania zitakazouzwa barani Afrika.
Aidha, Manongi amesisitiza mwongozo huo uwe nyenzo ya vitendo inayotoa taarifa zinazotekelezeka, akieleza kuwa muda wa kupata huduma au vibali unaoainishwa ndani yake unapaswa kuzingatiwa na taasisi husika. Amehimiza pia mwongozo huo kufanyiwa maboresho mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya taratibu, taarifa na mawasiliano ya maafisa wanaohusika, hatua itakayosaidia kupunguza pengo la taarifa, gharama zisizo za lazima na ucheleweshaji wa biashara.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA), Andrew Molle, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa wafanyabiashara kuhusu AfCFTA na kuwajengea uwezo wa kutumia fursa za soko hilo. Ameeleza kuwa Tanzania ina nafasi muhimu katika kuunganisha masoko ya kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, hivyo ni muhimu kuimarisha utekelezaji wa upendeleo wa ushuru, kupunguza vikwazo vya biashara na kuwajengea uwezo maafisa wa forodha ili bidhaa za Afrika ziweze kunufaika na makubaliano hayo.
Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na UNECA, ukiwa na lengo la kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kuelewa hatua za kufuata, mahitaji ya bidhaa, taratibu za kisheria na fursa za masoko katika biashara chini ya AfCFTA.










