Home Kitaifa Wadau Wa Maendeleo Waunga Mkono Ajenda Ya Sifuri Tatu Ya Rais Samia

Wadau Wa Maendeleo Waunga Mkono Ajenda Ya Sifuri Tatu Ya Rais Samia

Celebrating 25 Years of NHIF

Na.Mwandishi Wetu-ADDIS ABABA, ETHIOPIA

Wadau wa maendeleo ya sekta ya afya wameonesha utayari wa kuunga mkono ajenda ya sifuri tatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana barani Afrika,

FAHARI AFYA

Utayari huo umetangazwa na Viongozi na wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Maendeleo kwenye Mkutano wa Ngazi ya Juu uliolenga kujadili kuhusu utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Watoto na Vijana (RMNCAH) 2026–2030, uliofanyika Novemba 24, 2026, jijini Addis Ababa, Ethiopia, siku moja baada ya Rais Dkt. Samia kuzindua rasmi Mpango Elekezi huo katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika (CPHIA 2026).

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha dhamira ya kisiasa iliyowekwa kupitia mpango elekezi huo inatafsiriwa kuwa uwekezaji, maamuzi na utekelezaji wenye matokeo katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

“Sekretarieti itaendeleza ushawishi kwa viongozi wa Afrika, kuratibu mikutano ya kitaalamu, kuhamasisha rasilimali za kifedha na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha nchi zinatimiza ahadi zilizowekwa,” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.

Wakizungumza mara baada ya wasilisho la kitaalamu kuhusu Mpango Elekezi huo, wawakilishi wa taasisi na mashirika mbalimbali ya maendeleo, akiwemo Dkt. Shamma Khalifa Al Mazrouei, Mkurugenzi Mkuu wa Mohammed Bin Zayed Foundation for Humanity, Bw, Samwel Mulyanga Afisa Programu Mwandamizi wa Gates Foundation, Dkt. Sennen Hounton – Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Kanda ya Afrika Magharibi na Kati; Bi. Patricia Wamala, Afisa Programu kutoka Begginings Fund, Dkt. Tabinda Sarosh Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Pathfinder; Bi. Karoline Myklebust Mkurugenzi Mtendaji wa Laerdal Global Health; Dkt. Ntuli Kapologwe Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC); Serikali ya Norway, wameonesha utayari wa kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika pamoja na Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto katika kuunga mkono na kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya sifuri tatu ya Rais Samia.

Awali akizungumzia hali ya afya ya mama na mtoto barani Afrika, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), Profesa Diana Nambatya Nsubuga, amesema bara hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya vifo vya mama na watoto, ambapo asilimia 70 ya vifo vya wajawazito duniani hutokea Afrika, huku asilimia 58 ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano pia vikitokea katika bara hilo.

“Takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa afua za afya zenye matokeo makubwa ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma muhimu za chanjo” amesema Prof. Nsubuga.

Mshauri wa Kiufundi wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Dkt. Sunday Dominico, amesema kufikia lengo la Sifuri ya uzazi wa nyumbani tunahitaji vituo vya afya kuwa na watumishi wenye ujuzi, vifaa tiba na uwezo wa kutoa huduma bora, ikiwemo huduma za dharura na rufaa kwa wajawazito na watoto wachanga.

Ameeleza kuwa Sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga tutahitaji uchunguzi wa kina wa vifo vinavyotokea pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya kitaalamu, huku lengo Sifuri ya mtoto anayekosa chanjo likihitaji Serikali na wadau kushirikiana kuimarisha huduma za chanjo na kuwafikia watoto wote.likihitaji Serikali na wadau kushirikiana kuimarisha huduma za chanjo na kuwafikia watoto wote.

Akiwakilisha Tanzania katika mkutano huo, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nassoro Mazrui, amesema uzoefu wa Tanzania unaonesha kuwa uongozi madhubuti na uwekezaji endelevu katika sekta ya afya vinaweza kuleta matokeo katika kupunguza vifo vya mama na kuboresha huduma za afya.

Amesema takwimu za tafiti za afya na demografia zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito nchini vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2022, huku asilimia 80 ya wanawake wakijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya mwaka 2022.

Ameongeza kuwa matokeo ya awali ya utafiti mpya wa kitaifa yanaonesha kupungua zaidi kwa vifo vya wajawazito nchini, hatua inayokaribia lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu la kufikia chini ya vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.

Kupitia ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Africa CDC, Serikali na wadau wa maendeleo, ajenda ya sifuri tatu inalenga kuunganisha nguvu, uwekezaji na uwajibikaji ili kuhakikisha kila mama anajifungua salama na kila mtoto anapata fursa ya kuishi, kukua na kufikia afya bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!