

Tanzania na Uswisi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, ili kukuza uchumi wa mataifa hayo mawili.
Haya yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb.) Machi 06, 2025 wakati na alipokutana na na kuzungumza na Balozi mpya wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Nicole Providoli kuhusu kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji hususani katika uchakataji wa mazao.

Aidha, Dkt. Jafo amesema katika mkutano huo wamejadiliana jinsi ya kuwezesha uchakataji wa mazao kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao hayo ili kukuza kipato cha wakulima na biashara ya nje, wakati upanuzi wa biashara ukijikita katika kuongeza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uswisi kushirikiana na kupanua masoko yako.
Vilevile, wamejadiliana kuhusu kuimarisha uwekezaji kwa kuboresha Mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na marekebisho ya mifumo ya kodi, na ilikuleta ufanisi wa taasisi husika. Amesema Dkt Jafo.
Dkt Jafo pia amebainisha kuwa nchi hizo zimejadiliana kuhusu Marekebisho ya Sera za Kiuchumi hususani katika kuboresha sera ikiwemo Sera ya Viwanda ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (1996 – 2020), ili kuhakikisha sekta za kilimo, madini, na maliasili zinachangia zaidi katika uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake Balozi Providoli aliipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na amesisiiza kuwa Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo.