Home Kimataifa TANZANIA KUNUFAIKA NA PROGRAM YA BENKI YA DUNIA YA KUENDELEZA KILIMO

TANZANIA KUNUFAIKA NA PROGRAM YA BENKI YA DUNIA YA KUENDELEZA KILIMO

Na Benny Mwaipaja, Washington D.C

Tanzania inatarajiwa kunufaika na mpango wa Benki ya Dunia wa kuboresha mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo katika Bara la Afrika, kupitia program yake mpya ya kuendeleza kilimo ya AgroConnect, itakayogharimu dola bilioni 9 za Marekani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Dkt. Kibwe ambaye ni Mtanzania anayeshikilia nafasi hiyo kubwa katika Benki ya Dunia, alisema kuwa program hiyo itahusisha kuwasaidia wakulima kuboresha kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao yao na kuwaunganisha na masoko ya uhakika.

Alisema kuwa hatua hiyo si tu kwamba itaongeza usalama wa upatikanaji wa chakula, bali pia utaongeza upatikanaji wa ajira na kukuza uchumi jumuishi katika nchi wanachama wa Benki ya Dunia.

Alisema kuwa Benki ya Dunia inathamini ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Benki yake na Tanzania na kwamba itaendeleza ushirikiano huo kupitia mwelekeo mpya wa kisera ambapo msisitizo mkubwa umewekwa katika maeneo matano yenye kuziwezesha nchi wanachama hususan zilizoko katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuwekeza kwenye miradi itakayochangia kukuza ajira, kupitia sekta za kilimo biashara, ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli, nishati, afya, utalii na uzalishaji viwandani vitakavyo changia kuongeza thamani ya bidhaa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, pamoja na kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, alionesha furaha yake kwa Benki ya Dunia kuonesha utayari wake wa kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR), sekta ya madini, kilimo, elimu na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

Dkt. Mwamba alisema kuwa mpango wa Benki ya Dunia wa kuboresha sekta ya kilimo Barani Afrika unakwenda sambamba na vipaumbele vya Serikali ya   Tanzania kuendeleza sekta hiyo kupitia Dira ya Taifa ha Maendeleo ya 2050.

Uwekezaji wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania umefikia dola za Marekani bilioni 10.9 ambapo miradi 38 ya maendeleo ya kitaifa na kikanda inatekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji, elimu, nishati, ujenzi wa miundombinu ya barabara, na huduma za kijamii ikiwemo masoko na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Fedha na Mipango kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil na Kamishna Msaidizi wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!