📌Utekelezaji huo unafuatia maagizo ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, aliyetoa muda hadi Desemba 01, 2026.
📌TANESCO yakamilisha kazi Jumapili ya Novemba 15, 2026 ikiwa ni kabla ya muda ilioagizwa.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetekeleza maagizo ya Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, kwa kufunga transfoma mpya na kubwa yenye uwezo wa MVA 150 katika kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Ibadakuli mkoani Shinyanga, hatua inayolenga kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa umeme mkoani Katavi.

Hatua hiyo ni matokeo ya ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais aliyoifanya Oktoba 13, 2026 mkoani Katavi, ambapo akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, kuhakikisha TANESCO inaboresha hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Katavi ifikapo Desemba, 1 2026 ambapo TANESCO imekamilisha Jumapili ya Novemba 15, 2026.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme Mkoa wa Katavi baada ya marekebisho Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta amesema Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Lazaro Twange amrahidi mbele ya Makamu wa Rais hadi kufikia Disemba moja Mkoa wa Katavi utakuwa na umeme wa uhakika.

“Shukrani za wanakatavi zimwendee Mkurugenzi Mtendaji TANESCO kwa kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais kwa haraka sana chini ya muda ambao alituahidi wana Katavi,”amesema Kimanta.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Katavi, Mhandisi Florence Mwakasege amesema upatikanaji wa umeme Mkoa wa Katavi kwa hivi sasa umeimarika na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya maombi ya kuunganishiwa umeme kwani upo wa kutosha.

“Ilikuwa ikifika saa kumi na moja jioni au saa mbili usiku umeme unakatika kwa muda mfupi kutokana na kuzidiwa na mahitaji, lakini kwa hivi sasa changamoto hiyo imeisha baada ya kufunga transfoma kubwa ya MVA 150 kituo cha umeme cha Ibadakuli mkoani Shinyanga,”amesema Mhandisi Florence.
Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Katavi, Aman Mahela ameipongeza TANESCO kwa kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais kabla ya wakati ambao walikuwa wamepangiwa na kuhakikisha Mkoa wa Katavi unakuwa na umeme wa uhakika.

“Wafanyabiashara wa Katavi tunashukuru na kuwapongeza TANESCO kwa kukamilisha kazi hiyo kabla ya muda ambao umepangwa, natoa rai kwa wafanyabiashara wenzangu kuendelea kuiamini Serikali na inafanya kazi ya kuhudumia wananchi kwa wakati,”amesisitiza Mahela.
TANESCO ilianza kazi ya kufunga transfoma hiyo ya MVA 150 tangu Oktoba 27, 2026 na kukamilika Jumapili ya Novemba 15, 2026.

Kituo cha Badakuli ndicho kinacholisha umeme katika mikoa ya Tabora na Katavi. Kukamilika kwa ufungaji wa transfoma hiyo kunaongeza kiwango cha umeme kinachofika katika Manispaa ya Mpanda na maeneo jirani.









