Home Kitaifa SUDAN KUSINI YAOMBA USHIRIKIANO WA KIFORODHA NA TRA ILI KUTUMIA BANDARI ZA...

SUDAN KUSINI YAOMBA USHIRIKIANO WA KIFORODHA NA TRA ILI KUTUMIA BANDARI ZA TANGA NA DSM

Mamlaka ya Mapato ya Sudan Kusini (SSRA) imeomba ushirikiano wa kiforodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) utakaoiwezesha kutumia Bandari za Tanga na Dar es Salaam kupitisha mizigo yao badala ya bandari nyingine inazotumia kwa sasa.

Hayo yamejiri katika kikao cha pamoja baina ya Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, na Kamishna Mkuu wa SSRA, Bw. William Anyuon Koul, kilichofanyika Januari 22, 2026, katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam, kikilenga kuziwezesha mamlaka hizo mbili kushirikiana.

Kwa mujibu wa mazungumzo hayo, baada ya kuingia makubaliano ya ushirikiano, nchi ya Sudan Kusini kupitia SSRA itaweza kutumia Bandari za Tanga na Dar es Salaam badala ya bandari nyingine na kuwekewa mazingira mazuri yatakayohakikisha usalama wa mizigo na mapato kutokana na mizigo hiyo.

Kwa mara ya kwanza katika kikao hicho, Kamishna Mkuu wa SSRA alimwomba Kamishna Mkuu wa TRA apokee na kufikisha salamu kutoka kwa Mheshimiwa Jenerali Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, kwenda kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya majadiliano, Makamishna Wakuu hao walikubaliana kuendelea kuimarisha na kurasimisha ushirikiano kati ya mamlaka hizo mbili kupitia kuhitimisha Hati ya Makubaliano (MoU) ya kina itakayotoa mfumo wa jumla wa ushirikiano.

Kamishna Mkuu wa TRA amesema Hati ya Makubaliano hayo inatarajiwa kusainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Februari 2026 na kuanza kutekelezwa mara moja baada ya hapo.

Amesema Hati ya Makubaliano itatoa nafasi ya ushirikiano wa kimuundo katika ujenzi wa uwezo na maendeleo ya rasilimali watu, ikiwemo programu za mafunzo, kubadilishana utaalamu wa kiufundi, na mipango ya kuimarisha taasisi, kwa kuzingatia uzoefu na umahiri wa kila mamlaka.

Pia kuimarisha ushirikiano katika masuala ya forodha na kiutawala kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji na usimamizi wa ulipaji kodi katika tawala zote mbili.

Amesema eneo jingine ni kufanya kazi kwa pamoja kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili kwa kuongeza kiasi cha mizigo inayolenga Sudan Kusini kupita katika Bandari za Dar es Salaam na Tanga, kwa kutambua umuhimu wa kimkakati wa bandari hizo kwa biashara ya nje ya Sudan Kusini.

Aidha, Kamishna Mkuu Mwenda amesema katika majadiliano hayo Sudan Kusini imeomba kusaidiwa juhudi zinazolenga kutambua na kuwezesha upatikanaji wa eneo linalofaa la kushushia na kusafishia mizigo inayokwenda Sudan Kusini, ili kuboresha ushughulikiaji wa mizigo, taratibu za utoaji mizigo, na uratibu wa jumla wa masuala ya usafirishaji.

Aidha, kuendeleza ushirikiano wa karibu wa kiufundi katika mifumo ya kidijitali, ikiwemo kuunganisha Mfumo Mpya wa Forodha wa Tanzania (TANCIS) na Mfumo wa Forodha wa Kielektroniki wa Sudan Kusini, pamoja na kuingiza Mfumo wa Vibali wa Kielektroniki wa Sudan Kusini katika TANCIS ili kuwezesha uchakataji usio na vikwazo wa mahitaji ya forodha na udhibiti.

Maeneo yote ya ushirikiano yaliyokubaliwa yatatekelezwa ndani ya mfumo wa Eneo Moja la Forodha (Single Customs Territory), kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyaraka nyingine za kikanda zinazohusiana.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa SSRA, Bw. William Anyuon Koul, amesema ushirikiano baina yao na TRA utaiwezesha Sudan Kusini kutumia Bandari za Dar es Salaam na Tanga na kudhibiti ukwepaji wa mapato kupitia mifumo kusomana.

Amesema watumishi wa SSRA pia watanufaika kwa kupata mafunzo kupitia kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo na TRA, hali itakayoboresha utendaji katika mamlaka yao na kuwezesha biashara.

Hati hiyo imesainiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 22 Januari, 2026.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!