Home Kitaifa SERIKALI YAPIGA MARUFUKU ZAWADI NDANI YA BIDHAA ZA WALL PUTTY

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU ZAWADI NDANI YA BIDHAA ZA WALL PUTTY

Serikali, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imepiga marufuku utaratibu wa wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa za Wall Putty kuweka zawadi, fedha taslimu, vocha, kuponi, au vitu vingine tofauti na bidhaa yenyewe ndani ya vifungashio. Katazo hili linazingatia sheria na kanuni za viwango, ushindani wa haki, pamoja na taswira ya Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.

Serikali imesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wazalishaji na wasambazaji watakaokaidi agizo hili. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Vipimo (WMA) wamepewa jukumu la kuhakikisha kuwa bidhaa zote za Wall Putty zinazozalishwa zinakidhi viwango vilivyowekwa kabla ya kuingia sokoni. Aidha, msako mkali wa ukaguzi utaanza tarehe 1 Machi 2025, na wale watakaobainika kukiuka sheria watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo tarehe 7 Februari 2025, jijini Dodoma, inaeleza kuwa ukiukwaji wa Sheria ya Viwango (Sura ya 130), inayosimamia ubora wa bidhaa kupitia TBS; Sheria ya Vipimo (Sura ya 340), inayolinda usahihi wa vipimo na uzito wa bidhaa; pamoja na Sheria ya Ushindani (Sura ya 246), inayopinga upotoshaji wa watumiaji na ushindani usio wa haki sokoni, ni sababu kuu ya katazo hili.

Hatua hii inalenga kulinda haki za watumiaji, kuhakikisha ushindani wa haki katika soko, na kulinda taswira ya Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa kama vile EAC, SADC, COMESA, AGOA, na AfCFTA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!