
Serikali imetangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi kwa wastani wa asilimia 33.4, kutoka shilingi 275,060 hadi shilingi 358,322 kwa mwezi.
Akitangaza uamuzi huo leo, Oktoba 17, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Jakaya Kikwete, amesema kuwa kima hicho kipya kitaanza kutumika rasmi kuanzia Januari 1, 2026.
Waziri Kikwete amewataka waajiri wote nchini kuzingatia kima hicho kipya na kuhakikisha wanalipa mishahara kwa mujibu wa sheria, ili kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi.
Ikumbukwe kuwa awali, Serikali iliongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1, kutoka shilingi 370,000 hadi shilingi 500,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ustawi wa wafanyakazi nchini.