
Serikali imekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuelekeza nguvu katika kuzalisha wataalamu wabunifu, wenye ujuzi wa hali ya juu na uwezo wa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya utalii, kama sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kauli hiyo imetolewa Januari 20, 2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb.), wakati wa ziara yake ya kukagua eneo linalotarajiwa kujengwa Kampasi ya CBE Kilimanjaro, lililopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro. Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali wa serikali na chuo.

Amesema ujenzi wa kampasi hiyo unatarajiwa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kimuundo na kitaalamu zinazokabili sekta ya utalii nchini, kwa kuandaa wataalamu watakaobobea katika biashara ya utalii na shughuli zote zinazohusiana, ikiwemo ukarimu, ujasiriamali, masoko ya utalii pamoja na usimamizi wa biashara za utalii.
“Tunatambua mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika mapato ya Taifa na upatikanaji wa ajira. Ndiyo maana tunataka CBE izalishe wataalamu watakaoongeza thamani ya sekta hii, siyo kama waajiriwa pekee, bali pia kama wamiliki, wabunifu na waanzilishi wa makampuni na miradi ya utalii,” amesema Mhe. Londo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Tandi Lwoga, amesema Kampasi ya Kilimanjaro itakuwa kampasi ya tano ya chuo hicho nchini, na itachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza udahili wa wanafunzi katika nyanja za biashara na utalii.
Amesema kwa sasa chuo kina jumla ya wanafunzi 24,657, na kukamilika kwa kampasi hiyo mpya kutaongeza uwezo wa kudahili zaidi ya wanafunzi 2,000 kwa awamu.
Profesa Lwoga ameongeza kuwa usanifu wa majengo matatu ya awali tayari umeanza, yakijumuisha madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,000 kwa wakati mmoja, hoteli ya nyota tatu yenye uwezo wa kulaza wageni 52, pamoja na mabweni ya wanafunzi.
Amefafanua kuwa mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu (Higher Education Transformation Project), wenye thamani ya shilingi bilioni 17.4. Baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kifedha, ujenzi wa kampasi hiyo unatarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.








