Home Kitaifa SERIKALI YAENDELEA KUSISITIZA UMUHIMU WA KUZINGATIA VIWANGO , KONGAMANO LA BIASHARA LA...

SERIKALI YAENDELEA KUSISITIZA UMUHIMU WA KUZINGATIA VIWANGO , KONGAMANO LA BIASHARA LA VIWANGO 2026 .

 Na Mwandishi Wetu

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kama njia ya kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda unaolengwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kauli hiyo ilitolewa leo Juni 5, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa Viwango Business Forum iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika Ukumbi wa Mlimani City, ambapo wadau kutoka sekta mbalimbali walikutana kujadili nafasi ya viwango katika maendeleo ya biashara, viwanda na usalama wa walaji.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Profesa Mkumbukwa Mtambo, alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau wengine kuhakikisha viwango vinazingatiwa katika kila hatua ya uzalishaji na utoaji wa huduma.

Alisema viwango vina mchango mkubwa katika kuboresha ubora wa bidhaa na huduma, kuongeza uwezo wa viwanda vya ndani kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa, pamoja na kuimarisha imani ya watumiaji.

“Ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za udhibiti wa ubora ni muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi matakwa ya soko na mahitaji ya walaji. Kuzingatia viwango ni msingi wa kuongeza thamani ya bidhaa na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya viwanda,” alisema Profesa Mtambo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, Profesa Othman Chande Othman, alisema jukwaa hilo limeandaliwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wadau kubadilishana uzoefu na kujadili namna viwango vinavyoweza kusaidia kukuza ushindani wa bidhaa na huduma, kuimarisha biashara na kuongeza tija katika uzalishaji.

Alibainisha kuwa majadiliano hayo yanatoa fursa ya kubaini changamoto zinazokabili sekta mbalimbali na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua kwa manufaa ya uchumi wa taifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, alisema shirika hilo linaendelea kuimarisha juhudi za kusimamia ubora wa bidhaa na huduma nchini wakati likielekea kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Alisema katika kipindi hicho, TBS imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda afya na usalama wa watumiaji, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuchangia ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Dkt. Katunzi alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na TBS katika kujenga uchumi imara unaozingatia ubora, usalama na viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

Aidha, sehemu ya majadiliano katika jukwaa hilo ilijikita katika suala la usalama wa chakula, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Juni 7.

Wadau walisisitiza umuhimu wa kuhakikisha chakula kinachozalishwa, kusindikwa, kusafirishwa na kuuzwa kinazingatia viwango vya usalama ili kulinda afya za walaji na kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na chakula kisicho salama.

Kongamano hilo limewakutanisha wawakilishi kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za udhibiti wa ubora, wazalishaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo, likiwa jukwaa muhimu la kujadili mchango wa viwango katika kukuza biashara, viwanda na maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!