Home Kitaifa SALUM KULUNGE APITISHWA TENA KUWA MWENYEKITI WA GEREFA MKOA

SALUM KULUNGE APITISHWA TENA KUWA MWENYEKITI WA GEREFA MKOA

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA) leo kimefanya uchaguzi wake mkuu ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa GEREFA Mkoa wa Geita, Salum Kulunge, amepitishwa bila kupingwa kuendelea na nafasi hiyo. Wajumbe wa Kamati Tendaji waliochaguliwa ni Domisian Kabalega Butula na Kassim Mustapha Nangale.

Kwa upande wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, uchaguzi ulizua ushindani mkali kati ya wagombea watatu: Ally Ismail Twist, Leonard Mnenge Suluja, na Simon Joseph Shija. Suluja alipata kura sifuri, huku Twist na Shija wakigongana mara mbili kwa kura nane kila mmoja. Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa uchaguzi, Mwanasheria Kwandu Mapalala, alitangaza kuwa uchaguzi wa nafasi hiyo utafanyika tena ndani ya siku 60.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Salum Kulunge aliwashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kubwa kwake na kueleza kwa kina namna mchakato wa uchaguzi ulivyoendeshwa kwa uwazi kupitia kamati tendaji.

 “Ninawashukuru wajumbe wote kwa kuniamini kuendelea kuongoza chama hiki. Tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha maendeleo ya soka mkoani Geita yanaimarika.” Salum Kulunge – Mwenyekiti wa GEREFA Mkoa wa Geita:

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa shughuli hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili, amewataka wagombea na wajumbe kuchukulia uchaguzi huu kama sehemu ya demokrasia na sio uwanja wa uhasama.

 “Uchaguzi ni sehemu ya kutekeleza demokrasia. Ni muhimu kushindana kwa haki na mshikamano bila kujenga uhasama wa aina yoyote.” Paskasi Muragili – Mkuu wa Wilaya ya Bukombe:

Mwenyekiti wa uchaguzi, Mwanasheria Kwandu Mapalala, pia alisisitiza kwamba mchakato wa uchaguzi ulifuata misingi ya uwazi na haki, huku akiwataka wajumbe wote kushiriki kwa amani katika uchaguzi wa marudio.

 “Tunatarajia uchaguzi wa marudio kuwa wa haki, wa uwazi, na wa kiungwana kama mwongozo wa GEREFA unavyotaka.” Kwandu Mapalala – Mwenyekiti wa Uchaguzi:

Nao baadhi ya wajumbe walitoa maoni yao juu ya mchakato wa uchaguzi uliofanyika:

 “Nafasi ya uchaguzi huu ni nafasi ya kujifunza. Natumaini kuwa marudio ya uchaguzi yatakuwa bora zaidi.” Ally Ismail Twist – Mjumbe wa Mkutano Mkuu:

 “Tuliona uwazi katika uchaguzi huu, jambo ambalo linatia moyo kwa maendeleo ya soka letu mkoani Geita.” Joseph Kabote – Mjumbe wa Heshima wa GEREFA:

 “Tunawajibika kushirikiana kama viongozi wapya kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu katika mkoa huu.” Dunia Mrisho – Mjumbe wa Kamati Tendaji Wilaya ya Geita:

Uongozi mpya wa GEREFA unatarajiwa kuendeleza juhudi za kuboresha mpira wa miguu mkoani Geita, hasa kwa kuwapa nafasi vijana wenye vipaji kuonyesha uwezo wao kupitia ligi na mashindano mbalimbali. Wajumbe waliopitishwa wamesisitizwa kushirikiana kwa karibu ili kutekeleza mikakati ya maendeleo ya soka na kujenga mshikamano ndani ya chama.

Aidha, uchaguzi wa marudio kwa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa unatarajiwa kuwa wa haki na uwazi kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na GEREFA.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!