Home Kitaifa RC MTAMBI AWATAKA WANANCHI KUJIANDAA USHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

RC MTAMBI AWATAKA WANANCHI KUJIANDAA USHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Na Shomari Binda-Musoma

MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi amewataka wananchi kujiandaa na ushiriki wa uchaguzi wa serikali za mitaa

Kauli hiyo ameitoa leo septemba 23 ofisini kwake alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa mwaka 2024.

Mtambi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kushiriki uchaguzi huo.

Amesema kuanzia tarehe 11 hadi 20 oktoba 2024 kila mwananchi ajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili apate haki ya kupiga na kupigiwa kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwani mtu asipojiandikisha hataweza kupiga kura

Mkuu huyo amesema wananchi wasichanganye uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwaajili ya uchaguzi mkuu na huu uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa Mtambi amesema tarehe 15 agosti 2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa alitoa tangazo la uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 na kueleza kuwa utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024.

Kanali Mtambi amesema katika kuelekeza uchaguzi wa serikali za Mitaa yapo matukio muhimu ambayo ni pamoja na maelezo kuhusu uchaguzi wa serikali za Mitaa ambayo yatatolewa rasmi tarehe 26 Septemba, 2024 na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao ya utawala na uandikishaji wa wapiga kura litakalofanyika kwa siku kumi kuanzia tarehe 11-20 Oktoba, 2024.

Amesema kuwa kila mwananchi anapaswa kujiandikisha katika Kijiji, Mtaa au Kitongoji chake kwenye kituo ambacho atapigia kura na vituo hivyo vitaainishwa na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo hayo.

Amezitaja sifa za mwananchi anayepaswa kujiandikisha kuwa ni pamoja na awe raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, awe ni mkazi wa maa, kijiji au kitongoji ambapo uchaguzi unafanyika.

Amedai zoezi la kuchukua na kurejesha fomu kwa wanaogombea nafasi za uongozi ni tarehe 01 hadi 07 Novemba 2024 na zoezi la uteuzi wa wagombea litafanyika tarehe 8 novemba 2024 na kuwataka wananchi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Amezitaja nafasi hizo kuwa ni Mwenyekiti wa Mtaa, wajumbe wa kamati ya mtaa kwa halmashauri za miji na Manispaa; Mwenyekiti wa Kijiji, wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji kwa Halmashauri za Wilaya.

” Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa zitafanyika tarehe 20-26 Novemba, 2024 baada ya vyama vya siasa kuwasilisha ratiba ya kampeni zao kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya tarehe 14 novemba 2024 kwa mujibu wa mwongozo wa ratiba za uchaguzi”,amesema

Kanali Mtambi amevitaka vyama vya siasa kutoa ushirikiano kwa wasimamizi wa uchaguzi na viongozi wa Serikali waliopo katika maeneo yao na kuzingatia ratiba ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 ili uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa miongozo, sheria na kanuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!