Na Mwandishi Wetu.
Kila siku, wananchi hutoa Taarifa zao Binafsi kwa taasisi mbalimbali nchini ili kupata huduma za kijamii na kiuchumi. Ulinzi wa Taarifa hizo unahitaji siyo tu uwepo wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 (PDPA) bali pia uwepo wa wataalamu wenye uelewa na uwezo wa kuhakikisha matakwa ya PDPA yanatekelezwa ipasavyo.

Katika kuendelea kuimarisha Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) inaendesha mafunzo maalum kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi ikiwa sasa ni awamu ya nane, yanayofanyika Morena Hotel, Morogoro kuanzia leo Oktoba 07 hadi 08, 2026 ambayo yamewakutanisha zaidi ya washiriki 300 kutoka taasisi za umma na binafsi nchini kwa lengo la kuimarisha uwezo wao katika kutekeleza majukumu kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPA).
Maamuzi ya PDPC kutoa mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kujenga utamaduni wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini kwakua maafisa hao wana nafasi muhimu katika kuhakikisha taasisi zao zinaweka na kutekeleza mifumo inayozingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na hivyo kuboresha namna taarifa binafsi za wananchi zinavyokusanywa, kutumika, kuhifadhiwa na kulindwa.
Mafunzo haya maalum ya siku mbili ni sehemu ya jitihada za PDPC za kujenga uwezo wa wataalamu wanaosimamia Ulinzi wa Taarifa ndani ya taasisi zilizopo nchini na hivyo kuchangia katika kujenga mazingira salama na yenye uwajibikaji katika matumizi na usimamizi wa Taarifa Binafsi.

















