
-Yawawezesha mama na baba lishe Kigamboni kuhamia matumizi ya nishati safi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta mageuzi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umeendelea kuwawezesha mama na baba lishe kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida ili kuboresha afya zao, kulinda mazingira na kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia yaliyofanyika Novemba 24, 2026, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mhandisi Bruno Tarimo, amesema wakala huo umetambua umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.
Amesema mkakati huo, uliozinduliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Tarimo amesema PBPA imeamua kulipa kipaumbele kundi la mama na baba lishe kutokana na nafasi yao katika jamii na uwezo wao wa kuchochea mabadiliko ya matumizi ya nishati kupitia shughuli zao za kila siku.
Ameeleza kuwa kuhamia katika matumizi ya nishati safi si suala la kuhifadhi mazingira pekee, bali pia ni hatua muhimu katika kulinda afya za wafanyabiashara hao dhidi ya athari za moshi na kuboresha ustawi wao kiuchumi.
Ili kuwezesha mageuzi hayo kwa vitendo, PBPA imewakabidhi mama na baba lishe mkaa mbadala tani moja na nusu pamoja na majiko banifu 70 ili kuwapa fursa ya kutumia nishati hiyo na kujionea manufaa yake katika uendeshaji wa biashara zao.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mama na Baba Lishe Tanzania, Bi. Latifa Masasi, ameipongeza PBPA kwa kuwawezesha wafanyabiashara hao kuwa sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya nishati safi ya kupikia.
Amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuhamasisha wanachama wake kuachana na matumizi ya nishati chafu na kutumia teknolojia za kisasa za kupikia.
Naye baba lishe, Oswald Chanzi, ameishukuru PBPA kwa mafunzo hayo, huku akitoa wito kwa wadau kuhakikisha nishati mbadala zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendelea kuzitumia.
Kupitia kampeni hiyo, PBPA inaendelea kutoa mchango wake katika kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga jamii inayotumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya afya bora, mazingira endelevu na ustawi wa kiuchumi wa Watanzania.









