Home Kitaifa Daraja La Mgela Kufungua Fursa Za Kiuchumi Na Kijamii Wilayani Kilindi

Daraja La Mgela Kufungua Fursa Za Kiuchumi Na Kijamii Wilayani Kilindi

Celebrating 25 Years of NHIF

Kilindi, Tanga

‎Wananchi wa Kata za Kisangasa na Kibirashi wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wanatarajia kuondokana na changamoto za usafiri na mawasiliano zilizokuwa zikisababishwa na kuvuka mto Lukigula kufuatia ujenzi wa daraja la Mgela unaoendelea kutekelezwa na serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

FAHARI AFYA

‎Daraja hilo lenye urefu wa mita 20 linalounganisha vijiji vya Mgela na Nkoa linajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 923,142,475 fedha kutoka Mfuko wa Jimbo na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 70 huku mradi ukihusisha ujenzi wa daraja pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa mita 500.

‎Akielezea maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Dickson Mugisha kutoka TARURA wilaya ya Kilindi amesema kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa suluhisho la changamoto za usafiri zilizokuwa zikiwakabili wananchi na pia kutachochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

‎Amesema daraja hilo litakuwa kiunganishi muhimu kwa wakazi wa vijiji vya Mgela na Nkoa hasa wakulima na wafugaji ambao watapata fursa ya kusafirisha mazao na bidhaa zao kwenda sokoni kwa urahisi na kwa wakati.

‎Aidha, amesema daraja hilo litawawezesha wananchi kufikia huduma za kijamii ikiwemo zahanati, mahakama na shule bila vikwazo vinavyotokana na kuvuka mto hali itakayoongeza ufanisi wa shughuli za kila siku.

‎”Tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha za kutekeleza mradi huu ambapo Kukamilika kwa daraja hili kutaboresha mawasiliano kati ya kata hizi, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuwawezesha wananchi kupata huduma za kijamii kwa urahisi”, amesema Mhandisi Mugisha.

‎Kwa upande wake, Mwanyima Hossen mkazi wa Mgela amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa tangu daraja lao la awali lilipobebwa na maji hali iliyowalazimu kutumia kivuko cha muda ili kuendelea na shughuli zao za kila siku.

‎Amesema ujenzi wa daraja la kudumu ni faraja kubwa kwa wananchi kwa kuwa huduma nyingi muhimu za serikali zipo upande wa pili wa mto Lukigula zikiwemo shule ya msingi, mahakama na zahanati inayohudumia zaidi ya vijiji vinne.

‎Ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza usumbufu wa wananchi kufuata huduma za afya, elimu pamoja na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

‎Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Mgela Salum Hamza ameishukuru serikali kwa uwekezaji huo akieleza kuwa daraja hilo litakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijiji hicho.

‎Amesema wakulima watanufaika kwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa wakati huku wafanyabiashara wakipata urahisi wa kufikisha bidhaa kwa wateja jambo litakalosaidia kuongeza mzunguko wa biashara na kipato cha wananchi.

‎Aidha, ameiomba serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na miundombinu hiyo muhimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!