
*Asema Serikali kuendelea kuwashika mkono wawekezaji katika sekta ya miliki*
Wizara ya Ardhi kuja na Mamlaka ya Udhibiti wa Milki
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amezikaribisha kampuni na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini katika sekta ya milki ya makazi (real estate) akieleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya uwekezaji katika ardhi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua Maonesho ya Jukwaa la Majadiliano ya Sekta ya Milki ya Makazi (Tanzania Real Estate Expo – TAREX 2026), yaliyoandaliwa na Imperial Marketing and Communications Limited katika ukumbi wa Super Dome, jijini Dar es Salaam, na kusisitiza kuwa ardhi ni rasilimali muhimu kiuchumi ambayo mchango wake katika maendeleo unategemea namna inavyopimwa, kusajiliwa, kupangwa na kusimamiwa.
“Kwa sasa tunakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi kutokana na kutawanyika kwa makazi. Unaweza kukamilisha kusogeza huduma ya umeme katika eneo fulani, lakini baada ya muda mfupi unakuta kitongoji kingine kimeanzishwa mbali na eneo hilo. Hali hiyo inalazimu Serikali kupanga tena gharama za kupeleka umeme katika eneo jipya.“

“Vivyo hivyo, tunakutana na mahitaji ya kupeleka maji, kujenga shule, kujenga barabara na kusogeza huduma nyingine za kijamii katika maeneo mapya yanayoanzishwa. Endapo makazi yetu yangepangwa vizuri tangu mwanzo, Serikali ingeweza kutumia rasilimali chache zaidi kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema Serikali haitaki maendeleo ya sekta ya milki yapimwe kwa wingi wa majengo yanayojengwa pekee, bali pia kwa uwezo wake wa kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuimarisha mazingira ya makazi na kuhakikisha wananchi wanamudu gharama za nyumba, hususan vijana wanaohitimu vyuo vikuu na makundi mengine yanayokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa makazi.
“Takribani asilimia 70 ya wakazi wa mijini nchini wanaishi katika makazi yasiyo rasmi, hali inayohitaji ushirikiano mkubwa kati ya Serikali na sekta binafsi katika kurasimisha maeneo, kuendeleza makazi yaliyopangwa na kuongeza upatikanaji wa nyumba bora na ambazo wananchi wanamudu gharama zake. Hivyo ni fursa kwa wadau wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta hiyo,” ameongeza Waziri Mkuu.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kifedha na kuandaa miongozo itakayopunguza vihatarishi vya uwekezaji katika sekta ya milki ili wawekezaji wawe na uhakika wa mitaji.
“Idadi ya taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba nchini imeongezeka kutoka taasisi tatu zilizokuwepo awali hadi zaidi ya 29 kwa sasa, hatua inayopanua fursa za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa miradi ya milki. Uwepo wa Tanzania Mortgage Refinance Company ni hatua muhimu katika kuimarisha soko la mikopo ya nyumba nchini,” amefafanua Dkt. Mwigulu.
Kuhusu mipango miji, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji, waendelezaji wa miradi ya milki na wananchi kuzingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuondokana na ujenzi holela usiozingatia mpangilio, unaosababisha changamoto za upatikanaji wa huduma nyingine muhimu za kijamii zikiwemo barabara, maji, umeme na shule.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa sekta ya milki katika maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027, akieleza kuwa nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika hoteli, nyumba za kupangisha na miundombinu mingine ya malazi ili kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanapata huduma bora.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amesema wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza hatua za kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, ikiwemo kuja na mpango wa kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Milki ya Makazi (Real Estate Regulatory Authority – RERA), itakayosaidia kuweka mwongozo na kusimamia shughuli za sekta hiyo nchini.










