Home Kitaifa HALMASHAURI KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA SERA NA MWONGOZO WA KUREJESHA WANAFUNZI WALIOACHA SHULE

HALMASHAURI KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA SERA NA MWONGOZO WA KUREJESHA WANAFUNZI WALIOACHA SHULE

Celebrating 25 Years of NHIF

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umewakutanisha wataalamu kutoka halmashauri 10 nchini kujadili mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa sera na mwongozo wa kurejesha wanafunzi walioacha shule, kwa lengo la kuhakikisha changamoto zinazowakwamisha watoto kupata elimu zinapatiwa ufumbuzi.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika viwanja vya TGNP-Mtandao jijini Dar es Salaam, yamewashirikisha maafisa mipango, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa elimu kutoka halmashauri husika pamoja na wanajamii wanaotoka katika vituo vya taarifa na maarifa vya kata 12.

FAHARI AFYA

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwezeshaji wa Masuala ya Jinsia kutoka TGNP-Mtandao, Deogratius Temba, amesema lengo ni kuwaunganisha wataalamu hao ili kujadili namna halmashauri zinavyotenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza Waraka Na. 2 wa Elimu wa mwaka 2021, Mwongozo wa mwaka 2022 na Mpango Kazi wa mwaka 2025 unaohusu kuwarejesha wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali.

Amesema katika mafunzo hayo wamefanya tathmini ya hali ya utekelezaji wa sera na miongozo hiyo katika halmashauri husika, kubaini sababu zinazochangia wanafunzi kuacha shule, hususan wasichana, pamoja na kujadili namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

Temba amesema mafunzo hayo yamelenga pia kuweka mikakati ya kuhakikisha masuala ya kuwarejesha wanafunzi shuleni yanapewa kipaumbele katika mipango na bajeti za halmashauri kwa mwaka wa fedha 2027/2028.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya bajeti ya mwaka huo, hivyo ni fursa kwa halmashauri kuhakikisha mahitaji ya wanafunzi walioacha shule yanaingizwa katika mipango yao ya kifedha.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Robert Mwendwa, amesema mafunzo hayo yamemwezesha kupata uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuhakikisha wanafunzi wote walioacha shule wanarejea katika mfumo wa elimu na kuendelea na masomo.

Amesema baada ya mafunzo hayo atashirikiana na maafisa ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii pamoja na viongozi wa kata na jamii kuhakikisha wanafunzi walioacha shule wanatambuliwa na kurejeshwa shuleni.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa mpango huo unakabiliwa na changamoto ya mwamko mdogo wa jamii pamoja na ufinyu wa bajeti unaoathiri shughuli za uhamasishaji na ufuatiliaji wa wanafunzi katika maeneo mbalimbali.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa yenye kata 21 ina shule zilizotawanyika katika maeneo mbalimbali, hali inayofanya iwe vigumu kufika katika kila eneo kutokana na gharama za usafiri na ufuatiliaji.

Ameongeza kuwa baadhi ya shule hazina miundombinu rafiki kwa wanafunzi wa kike, ikiwamo vyumba maalumu vya kujisitiri, vyoo vya kutosha na huduma ya maji, changamoto zinazoweza kuchangia wasichana kushindwa kuendelea na masomo.

Mwendwa amesema pamoja na changamoto hizo, halmashauri inaendelea kutumia mapato yake ya ndani kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifundishia, hususan kwa wanafunzi wa kike.

Amesema hatua ya kwanza watakayochukua ni kuitisha vikao kuanzia ngazi ya halmashauri hadi shule na vijiji ili kutoa elimu kuhusu sera na miongozo ya Serikali na kuhakikisha jamii inaelewa vizuri utaratibu wa kuwarejesha wanafunzi shuleni.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Silvester, amesema halmashauri hiyo tayari imefanikiwa kuwarejesha baadhi ya wasichana na wavulana walioacha shule, ingawa bado wapo ambao wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto mbalimbali.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa walezi, hali duni ya maisha, ndoa na mimba za utotoni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu uwezekano wa wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni.

Amesema katika kukabiliana na hali hiyo, ataendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia kuhusu umuhimu wa watoto kurejea shuleni, kuimarisha elimu ya malezi chanya na kuhamasisha uanzishwaji wa vituo vya kulea watoto wadogo ili kuwasaidia wasichana wenye watoto kupata fursa ya kuendelea na masomo.

Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Lindi Manispaa, Mwandishi Nchimbi, amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kuwarejesha shuleni wanafunzi wote 29 waliokuwa wametambuliwa kuwa wameacha masomo na kwa sasa wanaendelea na elimu.

Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa wasichana walioacha shule fursa ya kurejea masomoni na kutimiza ndoto zao.

Ameongeza kuwa wanaendelea kupambana na mila na desturi potofu zinazochangia watoto wa kike kuacha shule, huku akisisitiza umuhimu wa kuwajengea wasichana ujasiri na kuwawezesha kutambua nafasi yao katika jamii.

Amesema wasichana waliopata ujauzito hawapaswi kuachwa nyumbani na kunyimwa fursa ya elimu, bali wanapaswa kupewa msaada unaowawezesha kurejea shuleni na kuendeleza ndoto zao za maisha.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya halmashauri na jamii katika kutekeleza sera na miongozo ya Serikali kuhusu urejeshaji wa wanafunzi walioacha shule, kwa msisitizo wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki na fursa sawa ya elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!