
Na Ashrack Miraji Lushoto Tanga
MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, Shabani Shekilindi ametoa onyo kwa watu ambao wanachonganisha wananchi na Serikali.
Shekilindi ametoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye mahafali ya wahitimu wa darasa la saba ambao katika Shule ya Msingi Mkurumuzi iliyopo kijiji cha Bombo kata ya Makanya wilayani humo.
“Ndugu zangu mimi sitokubali kwa kikundi cha watu wachache ambao wana uchu wa madaraka kuja kuwarubuni wananchi wa kata hii kwa sababu ya maendeleo ambayo yanatekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni makubwa na ni lazima tudumishe upendo,” amesema.

“Tusiwe wachoyo wa fadhila kwa kumshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo la Lushoto hasa kata ya Makanya, kata hii imepokea zaidi ya Sh.billion moja kwenye sekta ya elimu kwa kujengewa Shule ya Sekondari Bombo A, na sasa tunaanza kujenga mabweni ya kisasa kwa ajili ya watoto wetu ambao walikuwa wanapata changamoto ya elimu kwa kutembea umbali mrefu kwenda shuleni

“Sambamba na hayo Rais Samia amejenga kituo cha afya kikubwa na nimemuomba atujengee jengo la Mama na Mtoto katika kituo hili kuondoa kero kwa wakina mama ili waweze kupata huduma hiyo ya kujifungua na kliniki kwa ajili ya watoto wetu.
Nashukuru amekubali na muda si mrefu mwaka wa fedha 2024/2025 hatua za awali zitaanza hayo yote yanatokana na mimi mwakilishi wenu kwenda kuyasemea bungeni, leo Makanya inakwenda kuwa mji wa kisasa ukilinganisha na miaka ya nyuma,” amesema.

Mbunge huyo amewaomba wananchi kuwa na shukrani, huku akiwataka kujitokeza katika kugombea na kuchagua viongozi wenye uwezo kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi November mwaka huu.
Aidha Shekilindi amewata wazazi kuacha tabia ya kupeleka watoto mjini kufanya kazi za ndani, bali wawapeleke kusoma sekondari ili baadae wawe msaada kwa familia.

Mbunge huyo amesema iwapo kuna mzazi au mlezi atashindwa kulipa ada ya sekondari wawakilishe majina kwa mwenyekiti wa kijiji na diwani ili aweze kusaidia kulipa gharama husika.
“Mimi nitawasaidia wanafunzi ambao hawana vifaa vya shule, lengo letu kufika 2030 Dira ya Taifa ya Maendeleo kata ya Makanya iwe imekamilika kielimu kwa asilimia 100,” amesema



