Home Kitaifa MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA YATOA ELIMU YA SHERIA KWA WATENDAJI WA...

MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA YATOA ELIMU YA SHERIA KWA WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI GEITA DC

Mahakama Kuu Kanda ya Geita leo imetoa elimu ya masuala ya sheria kwa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha Watendaji wa Kata na Vijiji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Akifungua mafunzo hayo katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita – Nzera, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, amesema Mahakama imeona umuhimu wa kuwapatia watendaji hao elimu ya sheria ili waweze kusaidia jamii ipasavyo.

“Tunatambua nafasi muhimu ya watendaji katika mfumo wa utoaji haki na jinsi wanavyohusiana na shughuli za mahakama katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa,” alisema Mhe. Jaji Mhina.

Ameeleza kuwa Mahakama hiyo inatumia mifumo ya kisasa katika utoaji huduma, ikiwemo matumizi ya teknolojia badala ya karatasi, ili kuendana na maendeleo ya dunia. Pia, amesema katika Wiki ya Sheria, Mahakama imepanga kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu masuala ya kisheria.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Mpatanishi wa Migogoro Nchini, Ndg. Majaliwa Yohana, aliwakumbusha watendaji wa kata na vijiji kuhusu majukumu yao katika jamii, hasa kwenye masuala ya kisheria ili waweze kusaidia halmashauri kuepusha migogoro.

“Watendaji mnalo jukumu la kusimamia usalama, kudumisha amani, kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo, na kuhakikisha miradi ya serikali inatekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa bajeti na mipango ya maendeleo,” alisema Ndg. Majaliwa.

Naye Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Geita, Mhe. Frank Waane, aliwasisitizia watendaji hao kutekeleza amri za mahakama na kusuluhisha migogoro kwa mujibu wa sheria, kwani wao ni sehemu muhimu ya mhimili wa mahakama.

“Watendaji wa Vijiji na Kata wanatambuliwa kisheria chini ya kifungu cha 51 na 56 cha Sheria ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ya mwaka 2019 kama walinzi wa amani katika maeneo wanayohudumia,” alisema Mhe. Waane.

Katika mafunzo hayo, Msaidizi wa Sheria wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Mary Kazungu, aliwakumbusha watendaji hao majukumu yao mahakamani, hususan katika utoaji wa ushahidi kwa kuwa wao hupokea taarifa mbalimbali kuhusu migogoro katika maeneo yao.

“Watendaji mnapaswa kuwaelekeza wananchi kupeleka mashauri yao kwenye mabaraza rasmi ya usuluhishi wa migogoro yanayotambuliwa kisheria chini ya kifungu cha 102 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, ambayo yamewekwa katika ofisi za kata na siyo vijiji,” alifafanua Mhe. Kazungu.

Aidha, Afisa Uhamiaji, Koplo Isihaka Abasi, aliwataka watendaji hao kushirikiana na maafisa uhamiaji katika kudhibiti wahamiaji haramu kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Modest Burchad, aliishukuru Mahakama Kuu Kanda ya Geita kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yatasaidia kuwajengea watendaji uwezo wa kushughulikia masuala ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!