Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amepokea ugeni wa Waheshimiwa
Mabalozi wa Nchi za Umoja wa Ulaya waliowasili Mkoani humo kwa ajili ya kutembelea miradi ya Maendeleo
inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya iliyopo Mkoani humo.
Mara baada ya kuwapokea Mhe.Malima ameongoza Kikao kifupi( “Courtesy Call”) na kuwahakikishia Wahe.Mabalozi kuwa Mwanza ni salama na kuna fursa nyingi za uwekezaji na hivyo wasisite kutumia muda wao kwa ajili ya kujifunza na kuifurahia Mwanza.

Akiwatambulisha Wahe. Mabalozi Mhe.Malima amesema Wahe. Mabalozi wanatoka Umoja wa Ulaya, Ubelgiji, Finland , Ufaransa , Ujerumani , Ireland, Italia , Spain, Poland na Netherland.
Aidha, Mhe.Malima ameongeza kuwa wakiwa hapa Mwanza Wahe.Mabalozi watafanya Ziara ya kutembelea kwa kila Wilaya tarehe 24 hadi 26 Januari, 2023 wakianzia Nyamagana ambapo wataanza na
Miradi ya MWAUWASA (Mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba na Mradi rahisi wa utunzaji wa majitaka, uliopo Kirumba, Ilemela), na Maboresho ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, pamoja na Mradi wa ufugaji samaki kwenye vizimba ndani ya Ziwa Viktoria (Mpanju Fish Farm, iliyopo Nyegezi.

Wahe.Mabalozi watatembelea Mradi wa kuboresha michezo hususani viwanja vya michezo wa Sports
Charity, uliopo Sabasaba Ilemela. Pia kwa Wilaya ya
Sengerema watatembelea Mgodi Mkubwa wa dhahabu wa Nyazaga, Uliopo Kata ya Ngoma, Wilayani humo.
Kwa upande wa Misungwi, Mradi utakaotembelewa ni wa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Kikundi cha Mlimani Mining, kilichopo Shilalo Wilayani humo.

Mhe. Mkuu wa Mkoa ameshukuru Umoja wa Ulaya na wadau wake wa Maendeleo kwa mchango Mkubwa wanaoutoa wa kufadhili wa miradi ya Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.








