Home Kitaifa KATA YA BAGAMOYO KOROGWE TC YAPATA SHULE YA SEKONDARI

KATA YA BAGAMOYO KOROGWE TC YAPATA SHULE YA SEKONDARI

Na Yusuph Mussa, KOROGWE

HATIMAYE Kata ya Bagamoyo iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga imepata shule ya sekondari, na kuifanya Halmashauri hiyo yenye kata 11 kuwa na shule 10 za sekondari ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mbele ya Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Dkt. Alfred Kimea ambaye alitembelea Shule hiyo mara baada ya kupokea wanafunzi 80, Kaimu Mkuu wa shule hiyo Boniface Kinyemi, alisema shule ilipokea sh. milioni 470 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Kinyemi alisema zikiwa ni fedha za mradi wa SEQUIP kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika Kata ya Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Korogwe, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya Shule ya Sekondari Ngombezi ambayo ni shule jirani na Kata ya Bagamoyo, kwani kata hiyo haikuwa na shule ya sekondari.

Ujenzi wa shule hii unajumuisha ujenzi wa vyumba vinane (8) vya madarasa, ujenzi wa matundu 20 ya vyoo, ujenzi wa jengo la utawala, ujenzi wa maabara za masomo ya kemia na biolojia pamoja jengo la ICT (chumba cha compyuta). Ujenzi wa shule yetu umeanza kutekelezwa Machi 26, 2022 hadi sasa hatua mbalimbali zimefikiwa kama ifuatavyo;

Ujenzi wa jengo la utawala
limekamilika, ujenzi wa madarasa nane na ofisi mbili yamekamilika, maabara
zipo hatua ya umaliziaji, Jengo la ICT
hatua ya boma. Aidha hadi sasa kiasi cha sh. milioni 470 kimetumika”
alisema Kinyemi.

Kinyemi alisema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kumesaidia kutatua changamoto kubwa ya wanfunzi wa Kata ya Bagamoyo kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na baadhi kukosa kujiunga na elimu ya sekondari kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, kwani kata hiyo haikuwa na shule ya sekondari hapo awali.

Changamoto tulizonazo mpaka sasa ni kutokuanza ujenzi wa jengo la maabara ya fizikia, maktaba pamoja na umaliziaji wa jengo la ICT. Na hii imetokana na kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi kama vile nondo, batina cement.

Kwa niaba ya Ofisi ya Mkurugenzi, uongozi wa shule unaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi hii, kwani itapunguza changamoto kubwa ya wanafunzi kukosa vyumba vya kusomea pamoja na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni” alisema Kinyemi.

Naye Mbunge Dkt. Kimea, aliwataka walimu wa shule hiyo kuwa ya mfano kutokana na kujengwa kwa fedha za Serikali Kuu moja kwa moja, hivyo hata wanafunzi wa shule hiyo waoneshe uwezo kwenye ufaulu, huku pia akiwataka kulinda mazingira kwa kupanda miti.

Diwani wa Kata ya Manundu Rajab Mzige ambaye alikuwepo kwenye ziara hiyo, alisema shule hiyo ilikuwa iwe tawi la Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Manundu, na walianza kwa kujenga vyumba vitatu vya madarasa na kufikia hatua ya linta, lakini kulitokea mvutano sababu eneo hilo lipo Kata ya Bagamoyo, na kufanya maboma kukaa zaidi ya miaka 10 bila kuendelezwa.

Tunamshukuru Rais Dkt. Samia kuleta fedha na kukamilisha. Sisi Kata ya Manundu tulishaonesha njia kwa kujenga vyumba vitatu vya madarasa, na sasa shule imekamilika ikiwa ipo chini ya Kata ya Bagamoyo” alisema Mzige.

Kutokana na Shule ya Sekondari Semkiwa kuelemewa na wanafunzi wengi ikiwemo wa Kijiji cha Kwemasimba kilichopo Kata ya Vugiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, wananchi wa Mtaa wa Msambiazi, Kata ya Mtonga wanajenga shule ya sekondari ya pili kwenye Mtaa wa Msambiazi, na wameanza ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ili chumba kimoja kiwe ofisi, shule hiyo iweze kupokea watoto 2024″ alisema Komba.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Francis Komba alisema kwa sasa halmashauri hiyo yenye kata 11 ina shule 10 za sekondari, ambapo tisa ni za kata, na moja ya kitaifa, Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!