Home Kitaifa KAMISHNA MKUU WA TRA AMESEMA KITENGO CHA KUPAMBANA NA MAGENDO KITAFANYA KAZI...

KAMISHNA MKUU WA TRA AMESEMA KITENGO CHA KUPAMBANA NA MAGENDO KITAFANYA KAZI NA POLISI

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) BW. Yusuph Mwenda amesema kuanzia sasa oparesheni zote zitakazofanywa na kitengo cha kudhibiti wakwepa kodi (kitengo cha Fast) kilichopo chini ya TRA kitakuwa kikifanya kazi pamoja na Polisi.

Akizungumza wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa Marehemu Amani Kamguna Simbayao ambaye ni Dereva wa TRA aliyeuawa kwa kushambuliwa na Wananchi wakati akitimiza majukumu yake mwishoni mwa wiki Tegeta Nyuki Dar es Salaam, Kamishna Mkuu Mwenda amelipongeza jeshi la polisi kwa kuwashikilia baadhi ya washukiwa wa tukio hilo.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema wanatarajia waliokamatwa wote watachukuliwa hatua huku akiujulisha Umma kuwa, gari iliyokuwa ikifuatiliwa na Marehemu Amani na wenzake, ni kweli iliingizwa kimagendo na haikulipa kodi, na kodi ambazo zingelipwa zingefanya Maendeleo ya Taifa, na alichokifanya Marehemu ni kupigania kodi ikusanywe ili maisha ya Watanzania yaboreke.

Ningependa mjue, wanachokifanya watumishi wa TRA wanafanya kwa niaba ya Watanzania wote na hawa ni Ndugu zenu, hawastahili kufanyiwa alichofanyiwa Amani, wanastahili kupewa heshima kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya hivyo tunaomba Wananchi mshirikiane na TRA mtupe taarifa za ukwepaji wa Kodi.

Zipo taratibu mbili za usimamizi wa Kodi zikiwemo Sheria za usimamizi Kodi za ndani na sheria za usimamizi wa Kodi za kiforodha ambazo zinasimamiwa na Sheria ya Afrika Mashariki, ambazo nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki inazitumia na inatoa Mamlaka ya kufanya doria na ukamataji ambayo haihitaji kibali cha Mahakama.

Amesema Sheria hiyo ya kudhibiti magendo inaruhusu kuizuia mali na kuikagua, hivyo kazi waliyokuwa wakiifanya Marehemu na wenzangu ni halali na ni ya kisheria, kikanuni, na taratibu za ndani ziliruhusu wafanye jukumu hilo ambalo wakati wakilitimiza wapo walioamua kuvunja sheria kuzuia wajibu wao wa kufanya kazi.

Sisi tunalaani sana kilichotokea na baada ya msiba wa Marehemu Amani, Mhe. Mgeni Rasmi Sisi tunaendelea kutoa Elimu ili wajue kwamba kinachofanywa na TRA ni kwaajili ya Taifa na tunaendelea kutoa Elimu ya Haki na Mamlaka waliyonayo watumishi wakati wanatimiza wajibu wao” Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda.

Kwetu Sisi Marehemu ni Shujaa, amefariki wakati akitimiza majukumu yake siyo kwa familia yake ni kwa TRA na kwa Nchi, tutamkumbuka daima kwamba ni mmoja wa mashujaa, amefanya kazi yake kwa uadilifu na kwa uzalendo mkubwa, angeweza kukimbia na kutoroka pale alipokuwa lakini alikuwa anadhibiti mali ya Serikali, maana Yeye ni Mtumishi wa Wananchi” Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda akiwa msibani.

Najua ameacha Mke na Watoto wadogo, licha ya kuwepo kwa taratibu nyingine za Serikali, Sisi kama Mamlaka tutakaa tufanye utaratibu wa Mjane mwenyewe kumuwezesha aendelee kuishi, tutamuwezeshaje? Nimefurahi kuambiwa ni mjasiriamali na Sisi tuna huduma nyingi tunazotoa Mheshimiwa Waziri, hivyo tutaona namna tunavyoweza kumuajiri katika mojawapo ya huduma zinazotolewa TRA, suala la Elimu nakuachia Mhe. Waziri na hili ya Bima lipo ndani ya uwezo wetu, tutawakatia Bima Watoto waendelee kutibiwa kama ilivyokuwa hapo awali na hatutaiacha familia yake iteseke” Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!