Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limezindua kampeni ya wiki moja ya ukaguzi wa magari yanayotoa huduma za usafirishaji wa wanafunzi katika shule za Umma na binafsi Jijini humo kwa kuzingatia maeneo saba kwenye gari husika.
Katika kampeni hiyo iliyozinduliwa Juni 24, 2024; Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi (DCP) Wilbroad Mutafungwa amewataka Wakaguzi wa magari hayo kuzingatia mambo kadha ikiwemo uchakavu wa ‘bodi’ la gari, matairi, uwepo wa mikanda kwenye viti vya abiria, taa, leseni ya dereva iliyo hai, umahiri na ufanisi wa dereva ikiwemo ‘uoni wa dereva’ na uwepo wa mwangalizi wa wanafunzi ‘Matroni/Patroni‘ katika gari husika.
“Kuna mifano ya ajali mbaya za barabarani hasa kwa magari ya shule zilizopelekea vifo vya wanafunzi na pale ambapo uchunguzi ulifanyika ulionesha kwamba zimesababishwa na ubovu wa magari na uzembe wa madereva. Hatutaruhusu gari lisilokuwa na ubora kuendelea kubeba wanafunzi,” amesema Mutafungwa
Aidha, Kamanda Mutafungwa amemuagiza Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wakaguzi wa magari hayo wanakuwa na vifaa vinavyohusika ili kuhakikisha kila gari linakaguliwa kwa kuzingatia vigezo na maelekezo aliyotoa.
Kamanda Mutafungwa amebainisha kuwa ukaguzi wa magari ya shule zote zilizoko katika wilaya ya Nyamagana na Ilemela utafanyika katika eneo la maegesho ‘gereji’ iliyopo nyuma ya Stendi ya Nyamhongolo wilayani Ilemela huku wilaya nyingine wakitakiwa kupeleka magari yao katika Vituo vya Polisi katika wilaya husika kabla shule hazijafunguliwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Mkoani humo, Mrakibu wa Polisi (SP) Sunday Ibrahim amesema tayari magari zaidi ya 50 yamefikishwa katika gereji hiyo kwa ajili ya ukaguzi ambao ni bure; pia, amesisitiza kutembelea shule zote kwa ajili ya kubaini watakaokaidi zoezi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa shule, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Shule binafsi mkoani humo, Ezekiel Molel amewataka wenye magari kupeleka magari yao yakaguliwa huku akiahidi kutofumbia macho wale watakaokwepa ukaguzi huo muhimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Baraza la usalama barabarani Mkoa kwa Mwanza, Ferdinand Chacha amesema; “Magari yatakaguliwa sasa dereva uwe makini, ukiwa na gari nzuri lakini dereva hayuko makini ajali zitatokea tu. Kwa hiyo naomba madereva tuongeze umakini ili kupunguza ama kuondoa ajali kwa watoto wetu.”
Katika ukaguzi huo magari zaidi ya 50 yaliyofikishwa kituoni hapo yameanza kufanyiwa ukaguzi kabla ya kuruhusiwa kuanza kutoa huduma pindi shule zitakapofunguliwa Jumatatu Julai Mosi mwaka huu.