SERIKALI imesitisha zoezi la ukaguzi wa risiti za Kielekroniki (EFD) na ritani za kodi za Ongezeko la Thamani (VAT), iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kupitia mkoa wa kikodi wa Kariakoo, Jijini Dar es Salaam, wakati ukiandaliwa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo katika Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo.
Hayo yamesemwa kwa niaba ya Serikali, jijini Dodoma, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati akitoa maazimio ya kikao kati ya Viongozi wa Wafanyabiashara Tanzania, Viongozi wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo na Taasisi zinazosimamia masuala ya wafanyabiashara, kikao ambacho kiliitishwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na kuhudhiriwa pia na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, baadhi ya Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Prof. Mkumbo alisema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa wafanyabiashara katika kukuza uchumi wa nchi na kwamba itatumia kila njia kuhakikisha kuwa inaboresha mazingira ya kufanyia biashara kwa manufaa ya nchi na wafanyabiashara kwa ujumla.
Akifafanua kuhusu maazimio ha kikao hicho, Prof. Mkumbo alisema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka 2024, mamlaka ya Mapato Tanzania itaanza kutumia Mfumo mpya wa uwasilishaji nyaraka utakaosaidia wafanyabiashara kupata makadirio sahihi ya kodi.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Bw. Martin Mbwana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafanyabiashara nchini, Bw. Hamisi Livembe, wameipongeza Serikali kwa kuwasikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na kwamba hatua hiyo itaongeza ufanisi wa ufanyaji biashara katika Soko hilo linalotegemewa na wadau wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Elieza Feleshi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali na wawakilishi wa Taasisi zinazosimamia masuala ya viwanda na biashara.