
Na Monica Sibanda
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni ya Watanzania wote kwa kuwa imegusa makundi mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara, wanasiasa, na makundi maalum.
Rai hiyo ameitoa leo, Januari 10, 2025, wakati akifungua mkutano wa Asasi za Kiraia zilizokutana jijini Dar es Salaam ili kufanya mapitio ya rasimu ya kwanza ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Amesema ni muhimu kuwepo na majadiliano ya pamoja baina ya Serikali na wadau wa maendeleo, badala ya ukosoaji, ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa kuwa shirikishi.
“Serikali imejiandaa vya kutosha kusikiliza maoni yote yanayotolewa na wadau na wananchi ili kuhakikisha Dira 2050 inakuwa halisi na inayotokana na wananchi wenyewe,” amesema Nyongo.

Akizungumzia uzoefu wake akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, amesema amekutana mara kwa mara na kamati hizo za kiraia.
“Usipoelewa dhamira yao ya kukumbusha baadhi ya mambo, huenda ukafikiri kuwa wanaikosoa Serikali, jambo ambalo si la kweli. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujenga uelewa mpana wa mambo wanayoyajadili,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, ameipongeza Serikali kwa kuwajumuisha wadau wa asasi za kiraia katika uandishi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Aidha, Rutenge amehimiza umuhimu wa kukuza uchumi na kuwa na uchumi shindani kuelekea miaka 25 ijayo ili kutoa hakikisho la ustawi jumuishi na endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini (UNA-TANZANIA), Lucas Kifyasi, amesema utekelezaji wa dira hiyo unahitaji kipaumbele katika elimu, hasa ya teknolojia, kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda yanayotarajiwa kuimarika miaka 25 ijayo.