



Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeendelea kusisitiza msimamo wake wa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikitoa wito kwa watia nia wake kuondoa hofu ya uwezekano wa vitendo vya uonevu vinavyoweza kuvuruga ushindani wa haki.
Akizungumza mapema leo wakati wa zoezi la utoaji wa fomu za kugombea udiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Taarifa kwa Umma wa chama hicho, John Mrema, amesema hakuna sababu yoyote kwa wagombea wa CHAUMA kuwa na hofu au kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kuhofia kupokonywa ushindi au kunyimwa haki.
“Hatuwezi kuendelea kuruhusu chama kimoja kujitangaza bila kupingwa kwa kisingizio cha hofu. Tunapaswa kuwa na ujasiri, kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ili kuleta mabadiliko ya kweli nchini,” amesema Mrema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa CHAUMMA, Esther Fulano, amesema chama hicho kimejipanga vema kushiriki uchaguzi huo kwa lengo la kushinda na kuleta ushindani wa kweli katika uongozi wa nchi.
“Tutahakikisha kila eneo ambalo tutashinda linatangazwa kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria. CHAUMA haipo kwa ajili ya kushiriki tu bali kushinda na kuwahudumia Watanzania,” amesisitiza Fulano.
Chama hicho ni miongoni mwa vyama vya upinzani vinavyoendelea kujiimarisha kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025, kwa kuhimiza ushiriki mpana na maandalizi ya mapema kwa wanachama wake.








