Home Kitaifa CHANDE AWATAKA WAKULIMA KUTUMIA ELIMU YA FCC KUONGEZA THAMANI YA MAZAO

CHANDE AWATAKA WAKULIMA KUTUMIA ELIMU YA FCC KUONGEZA THAMANI YA MAZAO

Serikali imewataka wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali nchini kutumia elimu ya ushindani wa haki na ulinzi wa mlaji kama nyenzo ya kuongeza thamani ya bidhaa zao, kupanua masoko na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, alipotembelea banda la Tume ya Ushindani (FCC) katika Maonesho ya 33 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Nzuguni Dodoma.

Mhe Chande amesema elimu inayotolewa na FCC imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kuzalisha bidhaa zenye ubora unaoweza kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.

 “Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujenga mazingira rafiki ya biashara yanayozingatia ushindani wa haki, fursa sawa kwa washiriki wa soko na ulinzi wa maslahi ya walaji. Msingi huo unachochea uwekezaji, huongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha mchango wa sekta mbalimbali katika kukuza uchumi wa Taifa.”amesema Mhe.Chande

Hata hivyo amewahimiza wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kutumia kikamilifu elimu inayotolewa na FCC kwa kuzingatia sheria za ushindani, kuepuka vitendo vinavyopotosha soko na kujikita katika uzalishaji wa bidhaa bora zenye kukidhi mahitaji ya walaji.

“Hatua hiyo itaongeza thamani ya mazao, kuinua kipato cha wazalishaji na kufungua fursa zaidi za biashara ndani na nje ya nchi.”amesema 

Aidha, Naibu Waziri huyo ameipongeza FCC kwa kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za walaji na ushindani wa haki, akieleza kuwa juhudi hizo zinaimarisha mazingira ya biashara yenye uwazi na usawa kwa manufaa ya wazalishaji na watumiaji wa bidhaa na huduma.

Amesisitiza kuwa Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapa maarifa yatakayowawezesha kuongeza ubora wa mazao na bidhaa zao.

Ametoa rai kwa FCC kuendeleza kampeni za elimu nchini kote ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na fursa zinazotokana na soko lenye ushindani wa haki na hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!