
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Soka Wilayani Geita pamoja na Mkoa wa Geita na Mgeni Rasmi ambaye ni Afisa michezo wa WIlaya wakikata utepe kuhashiria ufunguzi wa ofisi

Ofisi ya Chama cha Soka Wilaya ya Geita

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita Salum Kulunge akitoa neno wakati wa Ufunguzi wa Ofisi ya Soka Wilaya ya Geita.

Mgeni Rasmi akikabidhi Kompyuta kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka WIlaya ya Geita.

Mwenyekiti wa chama cha Soka Mkoa wa Geita Salum Kulunge akikabidhi mpira.


Chama cha Soka Wilaya ya Geita (GEITA) kimefungua rasmi ofisi yake mpya kwenye mtaa wa Nyerere Road kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma za michezo. Hatua hii imelenga kuboresha utoaji wa taarifa mbalimbali za michezo na kusimamia maendeleo ya soka wilayani humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Geita, Ally Twist, alisema kwamba kufunguliwa kwa ofisi hizi ni sehemu ya mikakati madhubuti ya kuboresha mpira wa miguu katika wilaya. Alibainisha kuwa, kupitia ofisi hizi, mipango thabiti itakamilika, na vipaji vipya vya wachezaji vitakuwa sehemu ya juhudi za kukuza wachezaji wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mgeni rasmi wa tukio hilo, Afisa Michezo wa Mkoa wa Geita, Rodges Bahati, aliwapongeza viongozi wa soka wa wilaya hiyo kwa jitihada zao za kuendeleza mpira wa miguu mkoani. Bahati alisema viongozi hao wameonyesha maono makubwa ya kuhakikisha michezo inaimarika, huku wakiboresha timu zilizopo na kuzifanya kuwa bora zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita, Salum Kulunge, aliahidi kusimamia ligi za vijana kwa uadilifu mkubwa. Alisisitiza kwamba vijana watapewa fursa za kuonyesha vipaji vyao, hatua ambayo italeta mafanikio makubwa kwenye mchezo huo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Nyerere Road, Issa Dua Kabuli, aliwataka wadau wa michezo kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha vijana wanapata nafasi za kucheza katika timu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kabuli alisisitiza umoja na mshikamano kati ya viongozi na wadau ili kuleta mafanikio kwa jamii ya soka wilayani Geita.
Katika uzinduzi huo, harambee iliendeshwa kwa ajili ya kuinua mfumo wa Chama cha Soka Wilaya ya Geita, ambapo jumla ya TZS 131,500 zilipatikana na ahadi ya TZS 140,000 zilitolewa. Aidha, Mwenyekiti Ally Twist alikabidhi mipira kwa timu mbili zinazoshiriki ligi na vituo viwili vya kukuza vipaji. Timu hizo ni Nyankumbu Boys na Jamhuri FC, wakati vituo ni Jasper Academy na Geita TC Academy. Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Geita, Salum Kulunge, naye alitoa mipira 10 kusaidia kukuza vipaji vya vijana.
Pia, Mkurugenzi wa Twist Sport World, Ally Twist, alikabidhi kompyuta moja kwa ajili ya kurahisisha majukumu ya ofisi hiyo ya soka. Hatua hii imepongezwa kama mfano wa kushirikiana kwa manufaa ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu katika Wilaya ya Geita.