
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, Gabriel Nyasilu, amesema chama hakitamuonea haya kiongozi yeyote aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti au Mjumbe wa Serikali za Mitaa ambaye atashindwa kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao.
Nyasilu alitoa kauli hiyo katika kikao na wenyeviti na wajumbe wapya wa Serikali za Mitaa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa EPZA, mjini Geita.

Akizungumza katika kikao hicho, Nyasilu aliwataka viongozi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya chama na wananchi. Pia alisisitiza umuhimu wa uwazi katika usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma, akiwataka viongozi kusoma taarifa za mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu.
“Yeyote ambaye hatakuwa tayari kutekeleza wajibu wake kwa uwazi na uadilifu, hatutamvumilia. Tutahakikisha anachukuliwa hatua kwa maslahi mapana ya chama na wananchi,” alisema Nyasilu.
Aidha, alihimiza viongozi kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao ili kuimarisha imani ya wananchi kwa chama.