
Na Magrethy Katengu –Dar es Salaam,
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imesema ipo katika hatua za mwisho za kuandaa sheria na kanuni zitakazosimamia matumizi ya fedha za kidigitali nchini, hatua inayolenga kuwalinda Watanzania dhidi ya upotevu wa fedha na matumizi ya mifumo hiyo katika shughuli haramu.
Akizungumza leo Julai 10, 2026, wakati wa ziara yake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Gavana wa BOT, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema matumizi ya fedha za kidigitali yanaongezeka kwa kasi huku wananchi wengi, hususan vijana, wakivutiwa kuwekeza katika sekta hiyo.

Amesema BOT imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohitaji usimamizi madhubuti, ndiyo maana inaendelea kukamilisha mfumo wa sheria na kanuni utakaoweka mazingira salama kwa watumiaji wa fedha hizo.
“Nimeona watu wengi wakiliulizia sana suala hili, lakini bado ni eneo lenye changamoto zake. Nafahamu kuna vijana wengi wanaowekeza huko, lakini pia yapo malalamiko ya baadhi yao kupoteza fedha. Tunataka kuweka mazingira yatakayowalinda Watanzania wasipate madhara zaidi,” alisema Bw. Tutuba.
Pia Tutuba amongeza kuwa pamoja na fursa zilizopo, fedha za kidigitali zina vihatarishi vingi, ikiwemo uwezekano wa kutumika katika utakatishaji wa fedha na kufadhili shughuli za ugaidi, hivyo ni muhimu kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi.

Akizungumzia sera ya fedha, Bw. Tutuba amesema uamuzi wa BOT kuweka kiwango cha riba ya Benki Kuu katika asilimia 6.25 umezingatia hali ya uchumi wa nchi na lengo la kuhakikisha utulivu wa bei pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji.
Amebainisha kuwa hatua hiyo pia inalenga kuhakikisha kunakuwepo ukwasi wa kutosha katika mabenki ya biashara ili yaendelee kutoa mikopo kwa sekta binafsi, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Aidha, alisema kuanza kwa msimu wa mavuno kunatarajiwa kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania, jambo litakalowawezesha wakulima kupata bei nzuri za mazao yao na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Gavana amepongeza mafanikio ya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa Taifa kwa kuwakutanisha wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.









