
Serikali imesema Bajeti Kuu ya mwaka wa fedha 2026/27 ni ya kipekee kwa kuwa ndiyo bajeti ya kwanza itakayotumika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025-2030.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square jijini Dodoma, Bajeti ambayo itasomwa Bungeni Dodoma Siku ya Alhamisi, tarehe 11 juni 2026.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, Serikali inatarajia kutumia jumla ya shilingi trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo itaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Fedha hizi zitaelekezwa katika kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kuboresha mtandao wa barabara, kuimarisha huduma za maji, kuendeleza miradi ya nishati pamoja na uwekezaji katika rasilimali watu na maendeleo ya ujuzi,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, alisema kuwa bajeti hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ustawi wa wananchi na Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani ya shilingi trilioni 46.8 ili kugharamia sehemu kubwa ya matumizi yaliyopangwa katika bajeti hiyo.
Mhe. Balozi Omar aliongeza kuwa, kabla ya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2026/27, Serikali itatoa tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2025/26, akibainisha kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeendelea kufanya vizuri na kufikia malengo yaliyowekwa.
Aliongeza kuwa, Serikali imeendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa maandalizi ya bajeti kupitia Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi (Task Force on Tax Reforms) pamoja na Kamati ya Ushauri ya Ngazi ya Juu ya ‘Think Tank’, hatua ambayo imeongeza uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi ya sera za kodi.
“Upande wa maboresho ya kodi, Serikali imepokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, taasisi za elimu, jumuiya za wafanyabiashara, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi binafsi, ambapo kati ya mapendekezo hayo, 125 yalikubaliwa kama yalivyowasilishwa, 121 yalifanyiwa maboresho na kukubaliwa, huku 295 yakikataliwa baada ya kufanyiwa uchambuzi wa kina” alisema Mhe. Balozi Omar
Mhe Balozi Omar aliongeza kuwa, Lengo la maboresho hayo ni kukuza uchumi, kuongeza ajira, kupanua wigo wa kodi kwa kuvutia uwekezaji zaidi na wakati huo huo kupunguza mzigo wa kodi kwa walipakodi.
Mhe. Balozi Omar, alitumia fursa hiyo kuwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya maendeleo na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati.
“Tunajenga Taifa letu kwa pamoja. Serikali itaendelea kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kufuatilia kwa makini uwasilishaji rasmi wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 utakaofanyika Bungeni jijini Dodoma Juni 11, 2026, akisema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia matarajio ya wananchi na mahitaji ya maendeleo ya taifa.









