
📌 Nishati ya uhakika ni msingi wa uchumi imara, huduma bora za kijamii na maendeleo endelevu.
📍 Kamasi, Ukerewe – Mwanza
Wakazi wa Kisiwa cha Kamasi kilichopo katika Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, wamehimizwa kutumia fursa ya upatikanaji wa huduma ya umeme kwa kujitokeza na kujiunga na huduma hiyo ili kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku, kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha ustawi wa jamii.
Wito huo umetolewa na wataalamu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Kampuni ya Volt Afrika Limited pamoja na viongozi wa Serikali katika ngazi ya vitongoji na vijiji, waliofika kisiwani humo kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na kutumia huduma ya umeme kupitia mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika eneo hilo.

Katika zoezi hilo la uhamasishaji, wananchi wameelezwa namna umeme unavyoweza kuwa kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi kwa kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, ikiwemo biashara ndogondogo, ujasiriamali, shughuli za uvuvi na uchakataji wa mazao ya uvuvi, ambazo zina nafasi kubwa ya kuongeza kipato cha kaya na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kisiwa hicho.
Aidha, uwepo wa huduma ya umeme unatarajiwa kuleta manufaa makubwa katika sekta za kijamii, ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma za afya na elimu, kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuongeza fursa za shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme. Vilevile, matumizi ya nishati hiyo yanatarajiwa kuchangia juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa katika shughuli za kila siku.

Mradi huo wa umeme jua, unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutekelezwa na Kampuni ya Volt Afrika Limited, unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wateja 800 katika Kisiwa cha Kamasi, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa nishati ya uhakika na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande mwingine, wananchi wamehimizwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kujitokeza kuomba kuunganishiwa huduma ya umeme, wakitambua kuwa upatikanaji wa nishati ya uhakika si tu huduma muhimu kwa matumizi ya nyumbani, bali pia ni nyenzo muhimu ya uwezeshaji wa kiuchumi, uboreshaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya vijijini.
Mwisho









