
– ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI
-KUPOKEA WANAFUBZI JANUARY 2024
Na Shomari Binda – Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo ametembelea ujenzi wa shule 2 za msingi na sekondari zinazojengwa ndani ya jimbo.
Hatua za ujenzi huo zimemridhisha mbunge huyo na kuzipongeza kamati za ujenzi kwa ufatiliaji na usimamizi wake
Shule alizozitembelea ni shule mpya ya msingi Bweri na sekondari Bweri ambazo zimejengwa kwenye Kata ya Bweri.

Akizungumza mara baada ya kutembelea shule hizo amesema serikali imefanya kazi kubwa katika ujenzi wa shule hizo katika kuwasaidia wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Amesema wanafunzi wa eneo la Bweri Bukoba wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shuleni hivyo uwepo wa shule ya msingi mpya kwenye eneo hilo itawasaidia.

Mathayo amesema uwepo wa shule ya sekondari mpya ya Bweri itawapa nafasi wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani watapata nafasi hiyo.
“Niwashukuru sana kamati ya ujenzi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hizi za msingi na sekondari ambazo zinakwenda kuwasaidia watoto wetu.
“Mwakani januari 8 watoto wetu wanakwenda kuanza masomo kwa uhakika na ule umbali mrefu wa kwenda shuleni sasa haupo”, amesema Mathayo.
Mbunge huyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwaajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Bweri eneo la Bukoba wameishukuru serikali na mbunge Mathayo kwa ufatiliaji na kupatikana kwa shule hizo ambazo zitawasaidia watoto wao.








