Na Shomari Binda-
BAJETI ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2023/2024 imepanga kutengeneza kilometa 40 kiwango cha lami ya barabara ya Musoma-Makojo-Busekera.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 92 itajengwa kwa awemu 2 na awamu ya kwanza itaanza kwa kilometa 40.
Kwa sasa sehemu zenye lami kwenye barabara hiyo ni Musoma mjini-Buhare kilometa 5.9 pamoja na
Kusenyi-Kwikonero kilometa 5 eneo hili liko Musoma Vijijini.
Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini,Profesa, Sospeter Muhongo, ameshauri ujenzi wa kilometa 40 za barabara hiyo uendelee kwa kuanzia Kitongoji cha Kwikonero Kijiji cha Suguti hadi Busekera huku sehemu nyingine ianzie Kijiji cha Kusenyi hadi Musoma mjini.
Aidha Muhongo ameshauri pia apatikane mkandarasi mwenye uzuefu na mwenye vifaa vya kutosha ili kufanya kazi hiyo kwa ufasaha na ujenzi huo uanze mara baada ya bajeti ya mwaka 2023/2024 kuanza kutumika julai mosi.
“Barabara hii ni muhimu na itainua uchumi wa wananchi wa jimbo la Musoma vijijini na watanzania wote kwa ujumla.
“Inatakiwa kutafuta mkandatasi mwenye uwezo ili bajeti itakavyoanza kutekelezwa kazi ifanyike kwa haraka na kuweza kukamilika”,amesema Muhongo.
Amesema wananchi na viongozi wote wa chama na serikali wa jimbo la Musoma Vijijini wanaishukuru serikali kwa kufanya maamuzi mazuri ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
“Tunamshukuru sana Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio chetu cha miaka mingi na hatimae kuamua kutatatua tatizo hili sugu tunashukuru sana”, aliongeza.








