HALMASHAURI ya Itigi MKOANI SINGIDA imekuja na mpango wa kutokomeza baa la njaa katika Wilaya hiyo kwa kuibua Kampeni ya Ondoa Njaa Manyoni (ONJAMA) kwa kuhamasisha wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame kulingana na jografia ya eneo hilo.
Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Itigi Mkuu wa Wilaya ya Manyon Mhe.Kemilembe Lwota amesema serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuwapatia wananchi chakula cha bei nafuu katika maeneo yenye njaa ikiwemo wilaya ya Manyoni lakini amesisitiza kuwa utaratibu huo wa kutegemea serikali kuwapatia chakula ufike kikomo.
Amesema pamoja na jografia ya Wilaya hiyo kuwa na mvua zisizotabirika bado wananchi wanaweza kulima mazao ya chakula kama mihogo,mtama,uwele na mazao mengine ambayo yanaweza kuhimili mvua chache huku akiwataka madiwani kwenda kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kulima mazao ya aina hiyo ili kuepuka baa la njaa kujirudia katika wilaya hiyo.
Kwa upande mwingine DC.Lwota amewataka Madiwani, Divisheni ya Elimu na viongozi wa ngazi ya Kata kuhakikisha wanafunzi wote wanaotakiwa kuwa shuleni katika hatua ya elimu msingi na sekondari kuripoti shuleni mara tu shule zitakapofunguliwa.
Amesisitiza kuwa serikali imefanaya kazi kubwa ya kujenga miundombinu bora ya elimu ikiwemo vyumba bora na vya kutosha vya madarasa lakini changamoto imebaki katika zoezi la uandikishaji wa wanafunzi na kusema kuwa jambo hilo halikubaliki.
Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi Mhe. Hussein Simba amebainisha kuwa halmashauri hiyo kwa kiwango kikubwa inategemea makusanyo yanayotokana na mazao ya kilimo ambapo kufikia sasa makusanyo ya halmashauri ni takribani milioni 894 ikiwa ni sawa na asilimia 47.
Mhe.Simba amebainisha mikakati ya kuongeza nyanzo vingine vya mapato ikiwa ni pamoja na kujenga maegesho ya maroli na stendi ya magari katika mji wa Itigi na stendi ya magari katika kata ya Rungwa ambayo ujenzi wake unaendelea kufikia sasa kwa gharama ya shilingi milioni thelathini huku akishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais,Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati Ili kutoa huduma kwa wananchi.









