Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imekuja na mikakati mipya ya kuwawezesha vijana kujiamini na kujenga uthubutu wa kujiajiri baada kumaliza elimu zao za vyuo vikuu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga Wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe Mhe. Ameir Abdalla Ameir kuhusu vijana wanaomaliza vyuo vikuu na kusubiiri ajira kutoka serikalini katika kikao cha kumi cha baraza kumi la wawakilishi linaloendelea huko chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Amesema miongoni mwa mikakati inayofanywa na wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni pamoja na kuendesha mafunzo mbali mbali kwa vijana ili kubadilisha mitazamo ya kuweza kujiamini na kujenga uthubutu wa kujiajiri wenyewe, sambamba na kuanza hatua ya kuandika andiko la mradi la kufanya mikakati ya kufanyakazi karibu na taasisi za elimu kutengeneza mtaala wa elimu utakaozingatia masuala ya Ujasiriamli kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.
Ameongeza kuwa hadi sasa Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji kupitia programu zake za Uwezeshaji imefanikiwa kuwapatia mafunzo wananchi 4,171 kwa Unguja na Pemba katika fani mbali mbali zikiwemo Ujasiriamali, Ushoni, Umeme wa Jua, ufugaji wa nyuki, uokaji na usarifu wa matunda na mboga mboga.
“Kwasasa ZEEA inaendesha mashindano ya mpango wa biashara kwa vijana walioko vyuoni. Mashindano hayo huwapa fursa ya kupata mafunzo kwa wanaochaguliwa na zawadi ya mtaji (vifaa) kwa mshindi wa kwanza hadi watatu” alisema Soraga.
Pia Waziri Soraga amesema kupitia mafunzo ya kukuza ujuzi kwa Vijana, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji imefanikiwa kutoa mafunzo kwa Vijana 713 (wanawake 404 na wanaume 309) ambayo yamewawezesha kuthubutu na kujiajiri.
Akitolea ufafanuzi suala la mikopo Waziri Soraga amesema Kuwepo kwa fursa ya Mikopo ya wajasiriamali ya Mhe. Rais Dkt Hussein Mwinyi imeweza kuhamasisha Wananchi wa rika zote kupata mikopo na kujiajiri wenyewe na hatimae kujiinua kiuchumi na familia zao.








