
📌Ashiriki mjadala wa kuimarisha mifumo ya viwango kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania na barani Afrika;
📌 Asisitiza umuhimu wa kuoanisha viwango vya bidhaa ili kuongeza ushindani wa viwanda vya Afrika katika masoko ya kikanda na kimataifa.
📌 Ataja AfCFTA, EAC na SADC kuwa fursa muhimu za kukuza viwanda na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
📌 Aeleza jitihada za Serikali kuimarisha mazingira ya uwekezaji, uzalishaji viwandani na uwezo wa biashara ndogo na za kati.
Addis Ababa, Ethiopia.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya viwango na uzingatiaji wa masharti ya Afya ya Mimea na Wanyama (SPS) ili kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa barani Afrika na kupanua fursa za biashara katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Mhe Londo alikuwa akizungumza hayo Leo kwenye kikao cha 14 cha Jukwaa la Maendeleo ya Biashara Afrika (ATDF 2026), chenye mada Mtego wa Viwango (The Standards Trap), jijini Addis Ababa, Ethiopia na kunadi fursa za kibiashara zilizopo nchini Tanzania.

Mhe. Londo amesema nchi za Afrika zinapaswa kuoanisha viwango vya kitaifa na vya kikanda na kimataifa ili kupunguza vikwazo vya kiufundi vinavyozuia biashara na kurahisisha bidhaa kuingia katika masoko mbalimbali.
Amesema kuimarisha miundombinu ya ubora, ikiwemo upimaji, uthibitishaji, ukaguzi na uidhinishaji wa uwezo wa taasisi za upimaji, ni hatua muhimu katika kuhakikisha bidhaa za viwandani na mazao yanayozalishwa Afrika zinakidhi matakwa ya masoko na kusisitiza umuhimu wa kuzijengea uwezo biashara ndogo na za kati (MSMEs) katika masuala ya viwango, ubora, vifungashio na uthibitishaji wa bidhaa ili ziweze kushiriki kikamilifu katika minyororo ya thamani.
Akizungumzia fursa za kukuza biashara ya kikanda, Mhe. Londo amesema makubaliano ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yanatoa fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kupanua masoko, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kusisitiza juu ya matumizi sahihi ya fursa hizo yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na uwekezaji katika uzalishaji wenye tija na uongezaji thamani wa bidhaa.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na ugavi, pamoja na kuwezesha biashara kupata huduma za viwango na uthibitishaji kupitia taasisi husika zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA). Hatua hizo zinalenga kuongeza uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa bora, kuongeza thamani ya rasilimali za nchi na kupanua mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya Afrika na kimataifa.
Mkutano huo unawashirikisha Mawaziri wa Viwanda, biashara na mtengamano wa kibiashara kwa lengo la kujadili fursa za kibiashara kwa nchi za Afrika na namna ya killings bara la Afrika kibiashara kwa kutatua vikwazo vilivyopo ili kuongeza masoko.










