
Serikali imepanga kuhakikisha tiba asili inajumuishwa katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa huduma hizo kujumuishwa katika mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayolenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa Watanzania.
Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara ya Afya imeandaa mpango wa kuandaa dhifa ya uwekezaji katika dawa za tiba asili, ijulikanayo kama Asili Investment Gala 2027, itakayolenga kuhamasisha uwekezaji, tafiti, ubunifu na uzalishaji wa dawa za tiba asili nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengelwa, amesema mpango huo unalenga kuwaunganisha wadau mbalimbali, wakiwemo wawekezaji, taasisi za fedha, watafiti na watoa huduma za tiba asili, ili kujenga mazingira bora ya kuendeleza sekta hiyo na kuhakikisha inakuwa sehemu ya mfumo rasmi wa afya.
“Tulikwenda nchini India tukazungumza kwa kina kabisa namna ambavyo tiba asili inatoa mchango mkubwa kwa Watanzania, hasa kwenye tiba za Watanzania, na tukaona kwenye tafiti ambazo tumezifanya zaidi ya 60% ya Watanzania hutumia tiba asili. Zipo zile zilizosajiliwa, lakini zipo zile ambazo bado hazijapita utaratibu rasmi wa serikali,” amesema Waziri.
Waziri amebainisha kuwa dhifa ya uwekezaji katika dawa za tiba asili, ijulikanayo kama Asili Investment Gala, inalenga kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuendeleza tiba asili, uzalishaji wa dawa za tiba asili nchini, tafiti na ubunifu, pamoja na kujenga uwezo wa rasilimali watu ili kuhakikisha ujumuishaji wa tiba asili katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini.
“Mifumo rasmi inayotambuliwa kwa mujibu wa taratibu, lakini pia kwa mujibu wa sera yetu ya afya hapa nchini, kuna mikakati inaendelea na sisi tunawakaribisha wadau wa tiba asili mbalimbali, ikiwemo wawekezaji, viwanda na wale ambao bado hawajajisajili kufanya usajili wao mapema mara moja ili waweze kutambuliwa na kufikiriwa pale ambapo dawa zao zitakapoweza kuthibitishwa na wenzetu wa TMDA na mifumo mingine ya afya ambayo inaweza, ikiwa ni pamoja na MSD.“
Aidha, dhifa hiyo inatarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka 2027 ili kuwezesha wigo mpana wa ushiriki wa wadau. Dhifa hiyo itaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Wekeza katika dawa… wekeza katika dawa zetu za ndani za tiba asili.“
Dhifa hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka sekta binafsi, taasisi za fedha, jumuiya ya kidiplomasia, washirika wa maendeleo, taasisi za utafiti na wadau wa tiba asili.









