Home Kitaifa PDPC INAVYOTUMIA PDPA KULINDA TAARIFA BINAFSI ZA WANANCHI NA KUIMARISHA MAZINGIRA YA...

PDPC INAVYOTUMIA PDPA KULINDA TAARIFA BINAFSI ZA WANANCHI NA KUIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NCHINI

Celebrating 25 Years of NHIF

Katika uchumi wa kidijitali, taarifa binafsi zimekuwa rasilimali muhimu kwa shughuli za biashara, uwekezaji na utoaji wa huduma. Hata hivyo, thamani yake haiwezi kutenganishwa na wajibu wa kulinda faragha na haki za wananchi. Ulinzi wa taarifa binafsi hujenga uaminifu katika matumizi ya teknolojia, hupunguza hatari za matumizi mabaya ya taarifa na kuchangia mazingira yanayofaa kwa biashara na uwekezaji.

FAHARI AFYA

Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliridhia Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 (PDPA), iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2022 na kuwezesha kuanzishwa kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) tarehe 1 Mei, 2023. Hatua hizi zimeweka msingi wa kisheria na kitaasisi wa kusimamia ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi katika sekta za umma na binafsi.

Akizindua rasmi PDPC tarehe 3 Aprili 2024, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa faragha ni sehemu ya utu na staha ya mwanadamu. Aidha, alielekeza taasisi zote zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi kujisajili na kuzingatia sheria. Maelekezo hayo yalielekeza msisitizo si kwenye teknolojia pekee, bali pia kwenye uwajibikaji wa taasisi na haki za wananchi katika mazingira ya kidijitali.

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kusimamia utekelezaji wa sera na sheria katika eneo hili. Akifunga mafunzo ya Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (DPOs) jijini Arusha tarehe 5 Januari 2026, Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), alisisitiza umuhimu wa taasisi kujisajili PDPC na kuweka mifumo salama ya usimamizi wa taarifa. 

Kwa upande wa utekelezaji, PDPC chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, imeendelea kutoa elimu, kusajili wadhibiti na wachakataji wa taarifa binafsi, kushughulikia malalamiko na kusimamia uzingatiaji wa sheria. Akizungumza kwenye mafunzo ya DPOs jijini Mbeya tarehe 11 Februari 2026, Dkt. Mkilia alionya kuwa ukiukaji wa misingi ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa unahatarisha faragha, usalama na haki za wananchi. Tume pia ilitangaza kuanza kwa ukaguzi wa lazima tarehe 28 Agosti 2026 ili kuimarisha uzingatiaji wa matakwa ya sheria.

Hadi kufikia Oktoba 2026, zaidi ya taasisi 15,000 zilikuwa zimesajiliwa; malalamiko zaidi ya 445 yalikuwa yamepokelewa na kushughulikiwa; na vibali 121 vya usafirishaji wa taarifa binafsi nje ya Tanzania vilikuwa vimetolewa. Hatua hizi zinaonyesha kuimarika kwa taratibu za usimamizi, uwajibikaji na ufuatiliaji wa uchakataji wa taarifa binafsi nchini.

Uhusiano kati ya ulinzi wa taarifa binafsi na uwekezaji unatokana na hitaji la wawekezaji kuwa na uhakika wa usalama wa taarifa, uzingatiaji wa masharti ya kisheria na uwezo wa taasisi kulinda haki za wateja. Uwepo wa mfumo wa kisheria wa ulinzi wa taarifa unaweza kuongeza imani ya biashara zinazotegemea huduma za kidijitali na kubadilishana taarifa ndani na nje ya nchi. Hivyo, utekelezaji wa PDPA ni sehemu ya mazingira mapana yanayowezesha biashara, ingawa si sababu pekee inayoamua kiwango cha uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa uwekezaji nchini kwa mwaka 2021–2025 iliyotolewa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) tarehe 7 Januari 2026, miradi iliyosajiliwa iliongezeka kutoka 252 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.7 mwaka 2021 hadi miradi 915 yenye thamani ya dola bilioni 10.95 mwaka 2025. Mwaka 2024, thamani ya uwekezaji iliyotajwa ilifikia dola bilioni 9.3. Takwimu hizi zinaonyesha ukuaji wa uwekezaji katika kipindi ambacho Tanzania pia iliimarisha mifumo yake ya kidijitali na kisheria, ikiwemo ulinzi wa taarifa binafsi.

Ili manufaa ya mfumo huu yaendelee kuonekana, taasisi zinapaswa kujisajili inapohitajika, kuweka hatua za kiufundi na kiutawala za kulinda taarifa, kutoa taarifa kwa uwazi kuhusu matumizi ya taarifa na kushughulikia haki na malalamiko ya wananchi. Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wana nafasi muhimu katika kuratibu uzingatiaji wa sheria, kutoa ushauri kwa menejimenti na kufuatilia mienendo ya uchakataji wa taarifa ndani ya taasisi.

Wananchi nao wanapaswa kufahamu haki zao na kuwa waangalifu wanapotoa taarifa binafsi, hususani kupitia huduma za mtandaoni. Kwa kushirikiana na wadau, PDPC itaendelea kuimarisha elimu kwa umma, ukaguzi, usimamizi wa malalamiko na ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria. Hatua hizi ni muhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali unaoaminika, unaolinda utu na faragha ya mwananchi na kusaidia Tanzania kuwa na mazingira salama na yanayotabirika kwa uwekezaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!